Biden yuko Berlin kwa mazungumzo ya Ukraine na M. Kati – DW – 18.10.2024

Biden alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kufanya mazungumzo ya faragha na mshirika wake Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz katika ziara yake hiyo ya siku moja ya mjini Berlin yenye lengo la kujadili masuala kuanzia Ukraine hadi mzozo unaoenea Mashariki ya Kati.

Amesema atajadiliana na Scholz juu ya juhudi zinazoendelea za kuongeza msaada wa kijeshi kwa Ukraine na kuimarisha miundombinu ya nishati ya kiraia “kwa kuzifungua mali za Urusi zilizozuliwa”. Lakini pia wanajadili mzozo wa Mashariki ya Kati.

Kitisho cha baridi kali nchini Ukraine

Vyombo vya habari vimemnukuu akisema “Tunaingia kwenye kipindi cha baridi kali sana. Hatuwezi kusita lazima tudumishe msaada wetu. Kwa maoni yangu, lazima tuendelee hadi Ukraine ipate amani ya haki na ya kudumu kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ikiwa kwa mara nyingine tena, utu wao utakapojidhihirisha.” Alisema Biden

Ukraine | Uharibifu baada ya mashambulizi ya Urusi katika kijiji cha Yasenove
Bibi akiokota kuni kabla ya majira ya baridi kali katika eneo ambalo lilipigwa makombora hivi majuzi katika kijiji cha Yasenove, kusini mwa jiji la Pokrovsk, eneo la Donetsk, Oktoba 8, 2024.Picha: ROMAN PILIPEY/AFP

Katika mkutano huo Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alithibitisha tena nchi yake kujitolea kwa NATO na kusaidia Ukraine katika ushirikiano  wa pamoja na Rais wa Marekani Joe Biden. Scholz alimshukuru Biden kwa kutoa msaada muhimu baada ya Urusi kufanya uvamizi kamili kwa Ukraine 2022.

Matumaini ya kumalizika kwa vita vya Ukanda wa Gaza

Kadhalika Kansela Scholzalielezea matumaini yake kwamba kifo cha kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar kingefungua mlango wa kusitisha mapigano na kuachiliwa Mateka wa Israeli zaidi alisema. “Kwa kifo cha kiongozi wa Hamas Sinwa, ambaye alihusika na shambulio baya la kigaidi, tunatumai nafasi madhubuti ya kusitishwa kwa mapigano huko Gaza na makubaliano ya kuwaachilia mateka wa Hamas sasa yatafunguka.”

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanaungana na Biden na Scholz  Ijumaa hii kwa mazungumzo ya pande nne yaliyolenga zaidi jinsi ya kumaliza mapigano nchini Ukraine wakati vikosi vya Urusi vinasonga mbele katika upande wa mashariki.

Rais wa Ufaransa adokeza kuhusu mjadala kujikita katika suala la usalama

Itakumbukwa pia akizungumza na waandishi wa habari Alhamis, Rais Macron alisema kuwa suala kuu ambalo linawajumuisha wote katika mazungumzo ya leo ni hakikisho la kiusalama.

Soma zaidi:Rais wa Marekani Joe Biden amewasili mjini Berlin kwa ziara fupi

Tathmini inaonesha wazi kuwa hiki alichokifanya Biden mjini Berin, kinaweza kuwa ni ziara yake ya mwisho barani Ulaya chenye kuonesha ushahidi wa uhusiano wa karibu wa kikazi alionao na Kansela Scholz.

 

Vyanzo: DW/RTR/DPA

Related Posts