Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika kipindi cha mwezi Mei hadi Oktoba, 2024 kimefanikiwa kupata miradi 11 yenye jumla ya thamani ya takribani shilingi bilioni 4.5.
Hayo yameelezwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda kwenye mahafali ya 44 yaliyofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe Mjini Morogoro na kuhudhuliwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Vyuo pamoja na Balozi wa Msumbiji Nchini.
Profesa Chibunda amesema kuwa Chuo hicho kimeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kutekeleza program ya BBT (Bulding better tomorrow) hasa katika kutafuta vijana wa kupata ajira ya muda na endelevu.
“SUA tulipewa jukumu la kusaili na kujaza nafasi 2000 za wagani wa zao la pamba baada ya usaili wa awamu ya tatu Chuo kimeweza kupata wagani 700 na usaili wa awamu ya nne utaendelea hivi karibuni”. Amesema Prof. Chibunda.
“Kupitia program hii wahitimu wetu wa Shahada ya Kilimo na Vipando karibu wote wanauhakika wakupata kazi na hata wahitimu wa leo baadhi yao wamefanya usahili na kufaulu.”ameongeza Profesa chibunda.
Katika mwaka wa masomo 2024-2025 chuo kimedahili jumla ya wanafunzi wapya wa Shahada 5663 ambao wesajiliwa na kuizinishwa kujiunga na SUA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la SUA , Mhe Jaji Chande Othum amesema kuwa Baraza hilo liliidhinisha Mapitio wa Mpango wa Miaka 10 kuanzia mwaka 2024 hadi 34.
“Ili kuboresha mafunzo na kuongeza ujuzi kwa wahitimu, Baraza la Chuo limeendelea kuhimiza Chuo kutilia mkazo zaidi katika mafunzo kwa vitendo kwa kuboresha mashamba darasa,kalakana za uhandisi,maabara za mafunzo ya misitu ili kutoa fursa kwa wanafunzi na wadau wengine kupata mafunzo kwa vitendo ili waweze kuongeza maarifa”. Amesema Jaji Othuman.
Hii ni maafali ya 44 kwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ikiwa na jumla ya wahitimu 3061, kati yao wanaume 1650 na wanawake 1411 sawa na asilimia 46.1%