Jeshi la Israel, IDF limesema ndege zake zimeshambulia maficho ya silaha ya Hezbollah yaliyopo chini ya ardhi.
Mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP ameripoti moshi mkubwa mweusi uliotanda kati ya majengo mawili katika eneo la Haret Hreik, baada ya mashambulizi hayo.
Shambulizi hili limefanywa baada ya siku tano katika mji huo mkuu wa Lebanon na saa moja baada ya jeshi la Israel kuwaagiza raia kuondoka katika moja ya maeneo ya mji huo. IDF ilitoa onyo kupitia mtandao wa X ikisema inajiandaa kushambulia maeneo ya Hezbollah katika mji huo.
Netanyahu, amelikataa wazo la kusitisha mapigano na kuapa kuendelea kupambana na wanamgambo wa Hezbollah wakati Marekani ikiongeza shinikizo dhidi ya vitendo vya Israel katika vita vyake nchini Lebanon na Ukanda wa Gaza na hasa ikikosoa shambulizi la karibuni la bomu mjini Beirut huku pia ikitaka misaada zaidi kuwafikiwa watu wa Gaza.
Netanyahu alimwambia Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron jana Jumanne kwamba “anapinga usitishaji vita wa upande mmoja, ambao amesisitiza hautabadilisha hali ya usalama nchini Lebanon, hii ikiwa ni kulingana na taarifa ya ofisi yake.
Watu 20 wauawa katika mashambulizi tofauti ya Israel
Taarifa za Wizara ya Afya nchini Lebanon zimesema watu watano wameuawa baada ya Israel kushambulia jengo la manispaa ya mji wa Nabatiyeh kusini mwa Lebanon. Vyombo vya habari nchini humo aidha, vimeripoti kwamba Israel imefanya mashambulizi kadhaa kwenye mji huo na viunga vyake.
Duru za kiusalama zimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba meya wa manispaa hiyo ni miongoni mwa watu hao watano waliouawa, kufuatia mashambulizi hayo 11 ya anga yaliyofanywa na Israel, hii ikiwa ni kulingana na afisa mmoja wa Lebanon.
Na taarifa nyingine pia kutoka nchini humo, zimesema karibu watu 15 wameuawa katika mji wa Qana. Mji huo pia ulikumbwa na vifo vya raia katika mizozo ya huko nyuma kati ya Israel na Hezbollah.
Qana ilikabiliwa na vifo mwaka 1996 na 2006
Mnamo mwaka 1996, Israel ililishambulia jengo la Umoja wa Mataifa lililokuwa linakaliwa na mamia wa wakazi walioyakimbia makazi yao na kuua karibu raia 100 na kujeruhi wengine wengi, ikiwa ni pamoja na walinda amani wanne wa umoja huo.
Na kwenye vita vya mwaka 2006, shambulizi la Israel lilipiga jengo la makazi na kuua raia, theluthi miongoni mwao wakiwa ni watoto.
Na huko Ukanda wa Gaza, ambako Israel inapambana na Hamas, taarifa za Wizara ya Afya inayosimamiwa na Hamas, zinasema zaidi ya Wapalestina 42,409 wameuawa na 99,153 wamejeruhiwa tangu Israel ilipoanzisha mashambulizi katika eneo hilo, Oktoba 7, 2023.
Taarifa kutoka mjini Tel Aviv, zimesema Marekani kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni Matthew Miller, imeitolea wito Israel kuimarisha hali ya kiutu katika Ukanda wa Gaza, ndani ya kipindi cha siku 30.
Marekani imesema kinyume na hapo, kuna mashaka makubwa ya ukiukwaji wa sheria zake za misaada ya kijeshi, jambo ambalo linaweza kuhatarisha misaada yake kwa Israel, ikithibitisha ripoti za awali za vyombo vya habari, ingawa hakutaka kujibu swali kuhusiana na matokeo hasa, ikiwa Israel haitakubaliana na ombi hilo.