Mratibu wa Mradi wa EACOP kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Asiadi Mrutu akielezea maendeleo ya ujenzi wa mradi huo
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Taarifa hii imetolewa leo, Oktoba 18, 2024, na Mratibu wa Mradi wa EACOP kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Asiadi Mrutu, wakati Wajumbe wa Tume ya Kitaifa ya Mipango
ikiwa imeambatana na Bodi ya TPDC na Menejimenti ya TPDC ilipotembelea eneo la ujenzi wa Kiwanda cha kuweka mifumo ya kupasha na kutunza joto kwenye mabomba katika Kijiji cha Sojo, wilayani Nzega, mkoani Tabora.
Mrutu amesema kufuatia jitihada za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utekelezaji wa mradi huu kwa ujumla umefikia asilimia 45.5 ambapo shughuli za ujenzi zinaendelea katika maeneo mbalimbali kuanzia Mtukula Kagera mpaka Chongoleani Tanga na kwamba mpaka kufikia Oktoba 2024 Serikali kupitia TPDC imechangia mtaji wa takribani Shilingi Bilioni 977.6 kwenda kwenye Kampuni ya Mradi EACOP.
“Kiwanda hiki kinaendelea na uzalishaji wa mabomba ambapo mpaka sasa jumla ya mabomba yenye urefu wa kilomita 70.7 yamewekwa mifumo ya kupasha na kutunza joto. Ujenzi wa bomba na miundombinu yake unaendelea”,amesema.
Mpaka sasa mradi umeleta mafanikio makubwa ikiwemo fursa za ajira 7,584, manunuzi ya huduma na bidhaa za ndani ya nchi zenye thamani ya takribani Shilingi Bilioni 833.7, mapato kwa Serikali takribani Shilingi Bilioni 40, uhaulishaji wa teknolojia toka kwa wakandarasi”,ameeleza Mrutu.
Amefafanua kuwa Ujenzi wa Kiwanda cha kuweka mifumo ya kupasha na kutunza joto kwenye mabomba uliopo Kijiji cha Sojo Wilaya ya Nzega Mkoa wa Tabora umefikia asilimia 96 na ulizinduliwa rasmi na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko mnamo Machi 26, 2024. Kwa ujumla, mradi mzima wa EACOP umefikia asilimia 45.5.
“Pamoja na kuwa mwanahisa, TPDC inamiliki ardhi ya mkuza wa bomba na maeneo ya ujenzi wa makambi ambapo mpaka sasa tumefanikiwa kulipa fidia jumla ya Shilingi Bilioni 35.1 kwa wananchi 9,858 kati ya 9,927 sawa na 99.3%. Vilevile mradi umefanikiwa kujenga nyumba 340 za makazi mbadala kwa wananchi 294 waliopoteza makazi kwenye maeneo ya mradi. Serikali inaendelea kushirikiana na Wanahisa wengine ili kuhakikisha fedha za mradi zinapatikana kwa wakati na utekelezaji unaendelea ili kufikia malengo. Ujenzi unatarajia kukamilika katikati mwa mwaka 2026”,ameongeza Mrutu.
Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Mipango, Dk. Linda Ezekiel, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Ufundi na Madeni, ameeleza furaha yake kuhusu uwekezaji huu mkubwa, ukionyesha fursa kwa Watanzania.
Ameongeza kuwa, ziara hiyo ililenga kuona utekelezaji wa mradi kwa karibu na wamefurahishwa na kasi ya ujenzi, wakitarajia mradi kukamilika mwaka 2026 na kuanza kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.
Dk. Linda amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika mradi huu na kusema, “Nimefurahia kuona Watanzania wengi wameajiriwa na mradi huu unasimamiwa na wazawa.”
Mjumbe wa Bodi ya TPDC, Balozi Mstaafu Dkt. Peter Kallaghe, ameonyesha kuridhika na kasi ya ujenzi wa kiwanda cha Sojo, akisisitiza umuhimu wa mradi wa EACOP unaosimamiwa na Watanzania.
Amesema Bodi ya TPDC pamoja na Menejimenti itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi ikiwemo kuhakikisha mradi unakua wenye manufaa kwa Wananchi na jamii zilizopo karibu na maeneo ya ujenzi.
Wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Madeni, Bodi na Menejimenti ya TPDC imetembelea Kiwanda hicho ili kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko kuhakikisha Kiwanda kinaanza uzalishaji mabomba na kinakuwa chenye manufaa kwa Watanzania.
Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Kabaale (Uganda) hadi Bandari ya Tanga wenye urefu urefu wa kilomita 1,443 unatekelezwa na wawekezaji binafsi (Private Investors) kwa kushirikiana na Serikali za Tanzania na Uganda.
Wawekezaji katika Kampuni ya EACOP ni Kampuni ya TotalEnergies kutoka Ufaransa, CNOOC ya nchini China, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Kitaifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC).