Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Prof. Kithure Kindiki (52), ameteuliwa kuwa Naibu Rais wa Kenya, baada ya Bunge la Seneti kumtimua, Rigathi Gachagua, kwa kura jana usiku. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Tayari Rais William Ruto, amewasilisha jina la Prof. Kindiki bungeni na wabunge wamepiga kura ya kumthibitisha.
Awali, Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, aliwatangazia wabunge kupokea uteuzi huo katika Kikao maalum kinachofanyika leo Ijumaa.
“Nimepokea ujumbe kutoka kwa rais kuhusu uteuzi wa Profesa Kithure Kindiki kujaza nafasi katika afisi ya Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” amesema Spika Wetang’ula.
Baada ya wabunge kupiga kura kumthibitisha Prof. Kindiki Rais atamteua rasmi kuwa naibu wake.
Katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022, Prof. Kindiki alikuwa miongoni mwa waliopendekezwa kuwa mgombea mwenza wa Ruto, ambaye baadaye alimuacha na kumchagua Gachagua.
Rais Ruto alisema alimchagua Gachagua kwa sababu ya umri wake na alifikiri wangeelewana zaidi.
Kuidhinishwa kwa Prof. Kindiki kunatokana na uamuzi wa kutimuliwa kwa Gachagua jana usiku kwa Bunge la Seneti kumpigia kura, baada ya mjadala wa siku mbili ulioanza Jumatano wiki hii. Bunge hilo lilifikia uamuzi huo baada ya kupitia ushahidi wa kina wa tuhuma 11 zilizokuwa zinamkabili kiongozi huyo.
Aidha, tuhuma tano kati ya 11, ndizo zilizomwengua Gachagua madarakani.
Mfahamu Proffesa Kithure Kindiki
Abraham Kithure Kindiki alizaliwa tarehe 17 Julai 1972 katika kijiji cha Irunduni, kaunti ya Tharaka.
Prof. Kindiki ni wakili kitaaluma na mwanasiasa.
Kabla ya uteuzi huo, alikuwa anahudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa.
Amewahi kuwa seneti wa Kaunti ya Tharaka-Nithi, kuanzia 2013 hadi 2022, akiwa amechaguliwa mara mbili, mwaka 2013 na 2017.
Alipoingia Bunge la Seneti mwaka 2013, alichaguliwa kuwa kiongozi wa wengi na aliporejea tena kwenye bunge hilo mwaka 2017, alichaguliwa kuwa Naibu Spika wa Seneti kuanzia Agosti 2017 hadi 2020.
Kwenye nafasi ya uwakili, Prof. Kindiki anahudumu katika Mahakama Kuu nchini humo na pia alikuwa wakili katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akimtetea Rais Ruto, wakati huo akiwa Naibu Rais, chini ya utawala wa Uhuru Kenyatta.
Ruto na Kenyatta, walishtakiwa kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu baada ya kudaiwa kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, ambapo watu zaidi ya 1,000 waliuawa. Hata hivyo, mwaka 2016, kesi hiyo ilifutwa.
Prof. Kindiki alipata shahada ya Sheria (LLB) kutoka Chuo Kikuu cha Moi na Diploma ya Mafunzo ya Sheria kutoka Shule ya Sheria ya Kenya.
Pia ana Shahada ya Uzamili katika Sheria ya Kimataifa ya Haki za Kibinadamu na Demokrasia na Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kimataifa, kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini.
Mapema katika taaluma yake, Prof. Kindiki alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Moi.
Pia aliwahi kuwa Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Sheria ya Umma, katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Alipanda hadi kuwa Mhadhiri Mshiriki katika Shule ya Sheria katika taasisi hiyo hiyo.
Msomi huyo mashuhuri katika sheria za Kimataifa na haki za binadamu, amewahi kuwa mshauri wa mashirika ya ndani na kimataifa, yakiwamo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP).
Prof. Kindiki ni mwanachama wa Baraza kuhusu Mfumo wa Umoja wa Mataifa (ACUNS), Chama cha Kimataifa cha Utafiti wa Uhamiaji wa Kulazimishwa (IASFM), Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK) na Tume ya Kimataifa ya Wanasheria, Kenya (ICJ- K).
Prof. Kindiki ana Shahada ya Kwanza ya Sheria, kutoka Chuo Kikuu cha Moi, Diploma ya Uzamili ya Sheria kutoka Shule ya Sheria ya Kenya, Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M), na Shahada ya Uzamivu (PhD), katika Sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria nchini Afrika Kusini.
Watu wake wa katibu, wanamtaja kuwa mtumishi wa umma na Profesa wa Sheria mwenye rekodi nzuri na uzoefu mkubwa katika utawala, sera za umma, utungaji wa sheria, ushauri wa kisheria na masuala ya katiba katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Tarehe 08 Oktoba 2024, Bunge la Kitaifa, lilipiga kura ya kumwondoa madarakani Gachagua, baada ya kujadili hoja iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse.
Katika kura hiyo, wabunge 281 waliunga mkono hoja ya kumuondoa kiongozi huyo madarakani huku 44 wakipiga kura kupinga na mmoja akikataa kupiga kura.
Idadi hiyo ilizidi theluthi mbili ya kura zilizohitajika ili kupitisha uamuzi wa kumuondoa madarakani.
Miongoni mwa tuhuma zilizokuwa zinamkabili ni ufisadi, kumhujumu rais na kuendeleza mgawanyiko wa kikabila nchini humo, ambazo hata hivyo amezikanusha.
Gachagua ndiye Naibu Rais wa kwanza kuondolewa madarakani chini ya Katiba ya Kenya ya mwaka 2010.