SERIKALI imesema ili kukomesha ukatili wa jinsia na kwa watoto, itaendelea kushirikiana na jamii ili kufichua matukio hayo. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba, Dk. Franklin Rwezimula, ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam baada ya matembezi ya amani ya kupinga utekaji na mauaji dhidi ya watoto nchini pamoja na utoaji wa msaada wa sheria, yaliyoandaliwa na Wanawake wanasheria wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Dk. Rwezimula amesema kuwa Serikali itaendeleza jitihada za kutoa elimu kwa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwamo kutoa huduma za msaada wa afya ya akili kwa waathirika wa matukio ya ukatili.
“Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa haki jinai, ili haki itendeke kwa wakati wadau hawa ni pamoja na polisi, mawakili, na mwendesha mashataka wa Serikali,” amesema.
Aidha, amesema Wizara ya Katiba na Sheria, itaendelea kutoa ushirikiano kwa TLS ili kukomesha ukatilii huo.
Laetitia Petro, Makamu Mwenyekiti wa TLS, amesema jukumu la kuwalinda watoto ni la kila mmoja.
“Jamii yoyote inauhakika wa kuendelea kuwepo iwapo hali na mustakabali wa watoto wake ni salama na yenye kuwajenga kuwa na uhuru na udadisi kwa mazingira yanayowazunguka,”
Amesema kuwa ripoti ya 2020 ya Polisi inaonyesha ongezeko la asilimia 25.95 la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto “ripoti inasema kuwa mwaka 2020 kulikuwa na matukio 7,388 ukilinganisha na mwaka 2015 ambapo matukio yalikuwa 5,803.”
Amesema ripoti zinaonesha kwamba kila mwezi watoto 616 hufanyiwa vitendo vya ukatili.
Ameongeza kuwa ripoti ya haki za Binadamu ya mwaka 2023, inaonesha kwamba matukio ya kikatili 464 yalifanywa dhidi ya watoto.
Laetitia amesema licha kuwapo kwa sheria inayomlinda mtoto matukio hayo yanaongezeka kila mwaka.
Ameiomba serikali kuipa fedha TLS ili chama hicho kiweze kutoa huduma ya msaada wa sheria kwa watoto na wanawake, wanaofanyiwa ukatili.
Hilda Dadu mratibu wa wanawake watatezi haki za binadamu Tanzania, amesema jukumu la kukemea ukatilii wa jinsia ni la kila mmoja nchini.
“Tusimame kidete kukemea kila aina ya ukatilia wa jinsi bila kujali jinsia ya aina gani , tusimame kutetea usalama wa nchi yetu bila sisi nchi itakwenda vibaya,” amesema Dadu.
Amesema kuwa endapo wananchi na mawakili wakikaa kimya mauaji ya watoto yanaweza kuibua mauaji mengine.
Dadu amezitaka usikilizwaji wa kesi za ukatilii wa kijinsia na watoto ziendeshwe haraka ili haki ipatikane kwa wakati.