WANANCHI KIJIJI CHA NSEKWA WILAYANI MLELE WAIPONGEZA TARURA UJENZI WA BARABARA ZA LAMI

Mlele, Katavi

Wananchi
wa Kijiji cha Nsekwa, Kata ya Nsekwa katika Halmashauri ya Wilaya ya
Mlele mkoani Katavi wametoa pongezi zao kwa Serikali kupitia Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kutengeneza barabara za lami
Kilomita 3.73 ili kuwezesha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameishukuru Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupata barabara za lami katika kijiji chao
ambazo zimeweza kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.

Diwani
wa Kata ya Nsekwa, Mhe. Elijius Malando alisema, barabara hizo
zimewasaidia wafanyabiashara kufika kijijini kwao kununua asali, karanga
na mahindi ambapo kwa niaba ya wananchi ameishukuru serikali kwa
kujenga barabara inayoanzia makao makuu ya Wilaya kuja kijiji cha Nsekwa
kwani imewasaidia wananchi kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi.

“Wananchi
wamefurahi wanasafirisha bidhaa zao kwa urahisi na biashara
zimeongezeka watu wamefungua maduka, tunamshukuru Rais Samia kwa
barabara za lami ambazo zimewakomboa wajawazito waliokuwa wanajifungulia
njiani kwasasa wanafika hospitali ya wilaya kwa urahisi”, alisema Mhe.
Malando.

Naye, Mkazi wa kijiji cha Nsekwa Bw. Deogratius
Nicholaus alisema, hapo awali usafiri ulikuwa shida walikuwa wanatumia
nauli ya pikipiki shilingi 10,000 lakini sasa nauli ni shilingi 5000,
pia walikuwa wanatumia masaa mawili hadi matatu kufika mjini lakini sasa
wanatumia dakika 45 kufika mjini.

“Tunaishukuru serikali
kutupatia barabara sasa tunafanya biashara kwa urahisi, kabla ya lami
kulikuwa na michanga mingi, kutoka kijijini kwenda Inyonga tulikuwa
tunatumia masaa mengi kupeleka wagonjwa na kufuata huduma za kijamii
lakini sasa tunapita kwa urahisi”, alisema.

Kwa upande wake, Bi.
Anusiata Simon mkazi wa kijiji cha Nsekwa, ameishukuru serikali kwa
kujenga barabara ambazo zimerahisisha usafiri wa kutoka kijijini kwenda
Inyonga hadi Mpanda na amesema kwasasa wakiagiza bidhaa zinafika kwa
wakati na wanafanya biashara hadi usiku kwa sababu ya taa za barabarani
zilizowekwa ambazo zimeongeza usalama na kijiji kimependeza.

Meneja
wa TARURA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Paul Mabaya, ameishukuru serikali
kwa kuwapatia fedha takribani Bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa
barabara za lami Km 3.73 ambazo ni barabara ya Inyonga-Nsekwa Km 2,
Mapili-Utene Km1 na Uzega-Kafulu Km 0.73 zilizopo Kijiji cha Nsekwa
katika Halmashauri ya Mlele ambapo barabara ya Utene na Inyonga mradi
umekamilika asilimia 100 upo katika kipindi cha matazamio cha mwaka
mmoja.

 

Related Posts