Chadema yasema afisa wake mkuu alitekwa na kuumizwa vibaya – DW – 20.10.2024

Watu wasiojulikana walimteka nyara na kumjeruhi vibaya Aisha Machano, afisa wa ngazi ya juu wa chama cha upinzani CHADEMA nchini Tanzania, kabla ya kumtupa msituni, chama chake kilisema Jumapili. 

Tukio hili linatokea mwezi mmoja baada ya utekaji na mauaji ya kiongozi mwingine wa chama hicho. 

Visa hivyo vinavyoripotiwa huenda vikachafua taswira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya mpenda mageuzi, ambaye amekuwa akisifiwa kwa kupunguza ukandamizaji tangu kumrithi John Magufuli, aliyefariki akiwa madarakani miaka mitatu iliyopita.

Soma pia: Vyombo vya usalama vya Tanzania vyalaumiwa kwa mauaji

Mashirika ya haki za binadamu yanadai kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inawalenga wapinzani kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa Desemba na uchaguzi wa kitaifa mwaka 2025, ingawa serikali imekanusha madai hayo. 

Tanzania Tanga | Mazishi ya kada wa Chadema  Ali Mohamed Kibao
Mjumbe wa Sekreterieti ya Chadema Ali Mohamed Kibao alitekwa na kisha kukutwa ameuawa nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Hapa alikuwa anapelekwa kuzikwa nyumbani kwao Tanga.Picha: Ericky Boniface /DW

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Katibu wa Uenezi wa Umoja wa Wanawake, Aisha Machano, alitekwa nyara katika mji wa Kibiti, mashariki mwa nchi alipokuwa kwenye majukumu yake ya kikazi.

“Waendesha bodaboda (pikipiki) walimpata katika hali mbaya ya kiafya na katika maumivu makali,” chama hicho kilisema kwenye mtandao wa kijamii wa X.

CHADEMA imesema waliomteka Machano walitaka maelezo ya kina kuhusu nani aliwaagiza kuchoma nguo zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2023 mkoani Kilimanjaro.

“Alikimbizwa hospitalini kwa matibabu na amelazwa katika ,chumba cha upasuaji kwa matibabu zaidi,” chama kilisema.

Polisi Tanzania wamkamata Freeman Mbowe

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Polisi yaanzisha uchunguzi

Msemaji wa polisi David Misime alisema kuwa baada ya kupata taarifa kuwa Machano alipatikana katika msitu wa Kibiti, maafisa walianzisha uchunguzi wa tukio hilo.

“Tunaomba wananchi wawe watulivu kwani uchunguzi utatoa maelezo ya kina kuhusu tukio hilo, sababu za tukio hilo na watu waliohusika na tutawachukulia hatua za kisheria kulingana na ushahidi uliopo,” alisema.

Machano ni afisa wa pili mkuu wa upinzani kutekwa nyara na kuteswa ndani ya miezi miwili. 

Soma pia: Masauni atakiwa kujiuzulu kufuatia kifo cha kada wa CHADEMA

Ali Kibao ambaye ni mjumbe wa sekretarieti ya CHADEMA, alitekwa nyara kwenye basi na watu wenye silaha mapema mwezi uliopita alipokuwa akitokea Dar es Salaam kuelekea jiji la Pwani la Tanga.

Hali ya usalama ilivyoimarishwa Dar es salaam

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mwili wa Kibao baadaye ulipatikana nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ukiwa na ishara za kupigwa na kumwagiwa tindikali usoni, chama chake kilisema wakati huo.

Mnamo Septemba mosi, CHADEMA iliandaa maandamano kupinga kifo cha Kibao na madai mengine ya kutekwa na kupotea kwa watu binafsi na viongozi wa vyama vya upinzani jijini Dar es Salaam, maandamano amabayo polisi walizuia.

Mwezi uliopita Rais Samia aliamuru uchunguzi wa kifo cha Kibao na visa vyote vinavyohusiana nacho.

Related Posts