Samia hodari wa uchumi Afrika

*Tanzania: Kiongozi katika Mapambano dhidi ya umaskini Afrika

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Umaskini yemefanyika Oktoba 17, huku ikishuhudiwa Tanzania ikiwa kielelezo cha matumaini na maendeleo barani Afrika. Kwa mujibu wa takwimu za Afrobarometer, asilimia 51 ya Watanzania wanaamini kuwa serikali yao inafanya kazi nzuri au nzuri sana katika kuwaondoa watu kwenye umaskini.

Katika utafiti huo uliohusisha nchi 39 za Afrika Tanzania ni ya pili nyuma ya Zambia inayoongoza orodha hiyo ya raia wana imani na juhudi za serikali zao za kupambana na umaskini ikiwa na asilimia 54.

Mafanikio haya yanaonesha uongozi bora wa Rais Samia Suluhu Hassan katika mapambano dhidi ya umaskini na kuboresha hali za maisha ya Watanzania. Katika kipindi cha uongozi wake, Rais Samia ameweka kipaumbele katika kuimarisha uchumi wa ndani na kuweka sera zinazosaidia kupunguza umaskini, hususan kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu.

Wakati ambapo serikali nyingi za Afrika zinakabiliana na changamoto za kufikia matarajio ya wananchi wao, Tanzania inajitokeza kuwa mfano bora wa uongozi thabiti na sera madhubuti zinazoweza kuleta maendeleo.

Serikali inayoongozwa na Rais Samia imeonyesha kuwa kwa dhamira, mipango yenye malengo wazi na ushirikiano mzuri kati ya sekta mbalimbali, inawezekana kuboresha maisha ya mamilioni ya watu na kupunguza umaskini kwa kiasi kikubwa.

Katika juhudi zake za kupambana na umaskini, Rais Samia ameweka mkazo kwenye maeneo muhimu kama vile kilimo, afya, elimu na miundombinu. Hii imesaidia siyo tu kuinua kipato cha wananchi, bali pia kuimarisha upatikanaji wa huduma muhimu, hivyo kuondoa vikwazo vya kiuchumi kwa walio wengi.

Related Posts