Wanamgambo hao wameongeza kuwa walilifanya mashambulizi hayo katika kijiji cha Markaba kwa kutumia roketi na makombora karibu na kijiji cha Kfar Kila.
Katika Ukanda wa Gaza Wanajeshi wa Israel wameyashambulia makazi ya watu na na kuzizingira shule na makazi ya muda wakati wakitanua operesheni za kijeshi katika eneo la Jabalia Kaskazini mwa Ukanda huo. Wahudumu wa afya katika hospitali ya Indonesia kwenye Ukanda huo wamesema vikosi vya Israel viliivamia shule moja na kuwakamata wanaume kabla ya kulichoma jengo hilo kwa moto.
Soma zaidi: Israel yaivamia Gaza muda mfupi baada ya kumuua kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar
Moto huo ulizifikia jenereta za Hospitali hali iliyosababisha kukatika kwa umeme. Wakati mapambano yakiendelea Lebanon na Gaza, Waziri wa mambo ya Kigeni wa Marekani Anthony Blinken amesafiri kuelekea Mashariki ya kati katika juhudi za kuinusuru hali Mashariki ya kati baada ya kifo cha kiongozi wa kundi la Hamas Yahya Sinwar. Ziara hiyo ni ya 11 kwa Blinken Mashariki ya Kati tangu Oktoba 7.
Blinken kukutana na viongozi wa Mashariki ya Kati
Katika safari yake Waziri huyo wa Mambo ya Kigeni wa Marekani anatarajiwa kuzungumza na viongozi wa Mashariki ya Kati kuhusu umuhimu wa kusitisha vita Gaza, kuweka mipango ya maisha baada ya mzozo katika Ukanda wa Gaza, na suluhisho la mgogoro kati ya Israel na Hezbollah.
Ziara hiyo ya Blinken inafanyika baada ya mjumbe wa Marekani Amos Hochstein kufanya mazungumzo na maafisa wa Lebanon mjini Beirut. Katika mazungumzo hayo Hochstein amesema Marekani inashirikiana na Israel na Lebanon ili kupata namna ya kuumaliza kabisa mzozo.
Amesema kuwa Marekani imedhamiria kuataka vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hezbollah visitishwe mara moja wakati ikishinikiza kutekelezwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa linalowataka wapiganaji hao waondoke Kusini mwa Lebanon.
Hochstein amesisitiza kuwa azimio hilo namba 1701 lililovikomesha vita kati ya Hezbollah na Israel mwaka 2006 linapaswa kuwa msingi wa usitishaji mpya wa vita.