Tanzania kushirikiana na Uholanzi uzalishaji wa mbegu bora

Na Pamela Mollel,Arusha

Nchi za Tanzania na Uholanzi zimeanza kushirikiana katika teknolojia mpya za kutengeneza mbegu bora chotara za kilimo kwa ajili ya uzalishaji bidhaa za Mboga-Mboga kwa kiwango cha juu kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya masoko ya nje.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Stanslaus Nyongo amesema Tanzania kwa sasa inajikita zaidi katika kilimo cha uzalishaji, matunda, mbogana viungo kwa sababu ndilo eneo la uzalishaji linalowavutia Zaidi vijana pamoja na akina mama.

“Vijana hawapendi kilimo cha kawaida lakini wanavutiwa na kilimo cha bustani za mboga-mboga ambacho pia kinaelekea kuwa na soko zaidi nchini hivyo kutatua tatizo la ajira pamoja na kukuza uchumi,” alisema Nyongo.

Naibu waziri huyo alikuwa ni mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi upanuzi wa shamba maalum la kilimo cha kisasa kwa ajili ya kuzalisha mbegu linalomilikiwa na kampuni ya kimataifa yenye Makao yake makuu nchini uholanzi ijulikanayo kama Enza Zaden.

Shamba hilo la Enza Zaden Africa Limited linazalisha mbegu bora za kiwango cha kimataifa katika eneo la Nduruma, wilayani Meru mkoani Arusha, likiwa limeajiri watanzania zaidi ya 400.

Mbegu hizo chotara ni pamoja na zile za matango, matikiti, nyanya, Pilipili na mazao mengine ya mboga.

Balozi wa Uholanzi nchini, Wiebe De Boer aliyehidhuria tukio hilo amebainisha kuwa Enza Zaden ni kampuni inayochangia kuipa sifa kubwa nchi yake katika kukuza mbegu bora kwa ajili ya kuilisha dunia.

“Na inafurahisha zaidi kwamba sasa Enza Zaden wamewekeza Tanzania na watashirikiana na wananchi wa hapa katika kudumisha teknolojia bora za kilimo na uzalishaji wa bidhaa za mboga-mboga na kusafirisha nje,” alisema Balozi De Boer.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao kutoka wizara ya Kilimo, Nyasebwa Enock Chimagu amesema kuwa sekta ya kilimo, hususan katika eneo la uzalishaji mbegu, imeendelea kukua kwa kasi nchini.

“Sasa hivi bajeti ya wizara ya kilimo imeongezeka hadi 1.2 trillioni/- na kati ya hizo 80 billioni/- zimetengewa kwa ajili ya mbegu na utafiti, kwa sababu mbegu ndio kila kitu,” alisema Chimagu.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa utegemezi wa mbegu kutoka nje pia umepungua maana kwa sasa uzalishaji wa mbegu nchini umefikia tani 71,356 na kuifanya Tanzania ijitegemee kwa zaidi ya asilimia 78.6.

Mkurugenzi Mtendaji wa Enza Zaden, Jaap Mazereeuw amesema kuwa mbali la tawi la Tanzania, lililopo Arusha kampuni hiyo imewekeza katika nchi 26 duniani ambako imeajiri zaidi ya wafanyakazi 3000 huku ikidumu katika uzalishaji kwa zaidi ya miaka 85 sasa.

Maereeuw amesema mbegu hizi husambazwa katka nchi mbalimbali na hutumika kuzalisha bidhaa za vyakula vinavolisha zaidi ya watu Milioni 100 duniani

Meneja wa Opereshi katika shamba la Enza Zaden, Arusha, Gerald Matowo amesema kuwa mazingira ya Arusha ni mazuri kwa uzalishaji wa bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa.

“Hapa kuna maji safi ya asili, hali ya hewa nzuri, pamoja na kuwa karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro ili kurahisisha usafirishaji,” alisema Matowo.







 

 

Related Posts