TARURA YAKAMILISHA UJENZI WA DARAJA LA MSADYA, MKOMBOZI KWA WANANCHI WA MPIMBWE

Mpimbwe, Katavi

Serikali
kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha
ujenzi wa daraja la Msadya lenye urefu wa mita 60 na upana mita 10.5
pamoja na ujenzi wa barabara unganishi ya Kibaoni-Chamalendi-Mdede kwa
gharama ya shilingi bilioni 4.2 katika Halmashauri ya Mpimbwe mkoani
Katavi.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Paul Mabaya,
ameishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa daraja
la Msadya lenye uwezo wa kupitisha magari tani 30 ambalo limenufaisha
wananchi wa kata za Mwamapuli, Chamalendi, Ikuba, Kibaoni na Majimoto
kusafirisha mazao yao.

“Daraja hili limekuwa mkombozi, shughuli
kubwa hapa ni kilimo na ufugaji, kiasi kikubwa cha mpunga unaolisha nchi
yetu unatoka maeneo haya ya Mwamapuli, Lunguya na Chamalendi kuna
mashamba makubwa ya mpunga na mahindi hivyo daraja hili limerahisisha
usafirishaji wa mazao na mifugo”, alisema.

Aliongeza kuwa Wilaya
ya Mlele ina Halmashauri ya Mlele na Halmashauri ya Mpimbwe, amemshukuru
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya TARURA katika wilaya
hiyo kutoka Bilioni 1 hadi Bilioni 4 kwa mwaka na kwamba wanaendelea na
utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuwezesha wananchi kuzifikia huduma
za kijamii.

Naye, Mhe. Edward Madiliguntwe, Diwani wa Kata ya
Mwamapuli, ameishukuru serikali kwa kutengeneza daraja hilo
linalounganisha kata za Mwamapuli na Chamalendi ambalo limesaidia
wananchi kusafirisha mazao yao na kukuza shughuli za kibiashara na
uchumi.

“Kata hizi zinategemewa sana kwa kuzalisha chakula na
kukuza mapato ya hapa na Halmashauri nzima, tunamshukuru Rais Samia kwa
kutuletea fedha za daraja hili ambalo limekuwa mkombozi kwetu, zamani
wananchi walipata shida kuvuka mto huu ambapo walikuwa wanavuka kwa
kubebana lakini sasa wanavuka bila shida yoyote”, alisema.

Kwa
upande wake, Diwani wa Kata ya Chamalendi, Mhe. Yohana Maghembe alisema,
kabla ya daraja hilo wananchi kutoka Chamalendi ambao mahitaji yao yapo
Majimoto kipindi cha mvua walikuwa wanapata shida kuvuka na kupeleka
mifugo yao mnadani eneo la Majimoto, baada ya daraja kujengwa wananchi
wanasafirisha mifugo, mazao na bidhaa zao kupeleka viwandani na mnadani
bila shida ambapo amemshukuru Mhe. Rais na ameomba TARURA iendelee
kuongezewa fedha ili barabara ziendelee kuboreshwa zaidi.

Naye,
Bi. Jacquline Philipo mkazi wa kijiji cha Mwamapuli alisema, wajawazito
walikuwa wanapata shida kuvuka  walikuwa wanajifungulia njiani lakini
sasa wanaishukuru serikali kwa kuwajengea daraja ambapo kwa sasa
wanafika hospitali kwa wakati.

Bw. Sylvester Kibigi mkazi wa
Majimoto amesema, kabla ya daraja kujengwa kipindi cha mvua pikipiki
zilikuwa zinasombwa na maji, kwasasa wanapita bila shida baada ya daraja
na ameiomba serikali kuendelea kuwaboreshea barabara kutoka darajani
kwenda Mabambasi hadi Useja, barabara ya Chamalendi-Sentakichaa na
barabara kutoka darajani hadi Majimoto ili ziweze kupitika katika
nyakati zote.

 

Related Posts