Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo.
Jumuiya ya BRICS inayochukuliwa kama jukwaa la Kidiplomasia ilianzishwa miaka 15 iliyopita na mataifa ya Brazil, Urusi, China na India sasa limeendelea kutanuka na kuyajumuisha mataifa kama Afrika Kusini, Misri, Ethiopia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu. Nchi nyingine kadhaa tayari zimetangaza nia ya kujiunga na BRICS.
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva amelazimika kuifuta safari yake ya kuelekea Urusi kuhudhuria mkutano huo wa kilele wa BRICS. Daktari wa rais huyo wa Brazil mwenye umri wa miaka 78, Roberto Kalil amesema rais Lula alianguka na kujeruhiwa kichwani na kusababisha kuvuja damu kidogo kwenye ubongo na hivyo anatakiwa kuwa chini ya uangalizi na kuepuka kwa muda safari za ndege za masafa marefu.
Putin ampokea rais wa UAE
Rais wa Urusi Vladimir Putin amempokea rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kusema mahusiano kati ya mataifa hayo mawili ni sawa na ushirikiano wa kimkakati.
Putin alimualika chakula cha jioni Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan na wawili hao wanatarajia kuzungumzia mzozo wa Mashariki ya Kati na vita vya Ukraine katika mazungumzo yao rasmi hivi leo kabla ya mkutano wa BRICS.
Putin amemshukuru pia Al Nahyan kwa juhudi za upatanishi katika kubadilishana wafungwa wa vita na Ukraine, ambapo mabadilishano ya hivi punde yalifanyika siku ya Ijumaa, na kila upande ukiwarejesha nyumbani wafungwa wa kivita 95.
Malengo ya Moscow kuitanua BRICS
Urusi inalichukulia kwa umuhimu mkubwa suala la kuitanua BRICS na kulifanya kuwa nguzo ya sera yake ya kigeni. Kremlin inatumai BRICS itakabiliana na ushawishi wa mataifa ya Magharibi. Hata hivyo Marekani imetupilia mbali wazo kwamba BRICS inaweza kuwa mpinzani katika siasa za kijiografia.
Mazungumzo hayo ya BRICS yanatazamiwa kuangazia mzozo unaoongezeka huko Mashariki ya Kati, pamoja na wazo la Putin la kuanzisha mfumo wa malipo utakaoongozwa na mataifa ya BRICS ili kuleta ushindani kwa mfumo wa SWIFT, ambao ni mtandao wa kimataifa wa kifedha ambao benki za Urusi zilizuiwa kuutumia mnamo mwaka 2022.