ZAIDI YA WASHIRIKI 3,000 WASHIRIKI UZINDUZI WA KAMPENI YA TUWAAMBIE KABLA HAWAJAHARIBIWA ARUSHA.

Na. Mwandishi Jeshi la Polisi Arusha.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limezindua kampeni ya tuwaambie kabla hawajaharibiwa kwa lengo la kuongea na wanafunzi kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu kwa ajili ya kuwaelimisha juu ya kujitambua ili kujiepusha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili.

Akizungumza katika uzinduzi huo ambao umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000, Katibu Tawala Msaidizi viwanda Biashara na uwekezaji Mkoa wa Arusha Bw. Frank Mbando ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amewataka wanafunzi kuhakikisha wanajitunza vyema na kuwa makini na rika walilopo kwa kujiepusha na vitendo ambavyo vitaharibu maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Aidha amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu kwa kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bure yenye ubora ambapo amesema hadi sasa zaidi ya shilingi bilioni saba zimeshatolewa tangu serikali ya awamu ya sita iingie madarakani.

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi SP Happiness Temu amesema lengo la kampeni hiyo ni kuwatahadharisha wanafunzi wa shule za awali Msingi, Sekondari na vyuo vya juu kuacha kuiga tabia mbovu ambazo hazina tija katika ustawi wa Maisha yao ya kila siku na masomo.

SP Temu amebainisha kuwa kupitia elimu ambayo itaenda kutolewa itasaidia kujenga taifa litakalokuwa na kizazi chenye maadili mema na raia wema wanaojitambua kabla ya kupitia mapito ya ukatili.

Kamanda wa Kikosi Cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua amesema dhima ya Jeshi la Polisi kupitia kampeni hiyo ni kuhakikisha linayafikia makundi yote ya wanafunzi kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo vya ngazi zote kuzungumza nao kuwapa elimu ya kujitambua mapema.

Katika uzinduzi wa Kampeni hiyo Washiriki zaidi ya 3,000 ambao ni Jeshi la Polisi, Shule zaidi ya 10, vyuo 12 pamoja na Wananchi walishiriki.







Related Posts