Blinken anakutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant na maafisa wengine wa juu wa Israel mwanzoni mwa safari ya wiki nzima ambayo pia itampeleka Jordan na Qatar.
Maafisa wa Marekani wamesema Blinken ataangazia mipango ya kuijenga upya Gaza na utawala katika eneo hilo baada ya vita, jambo ambalo ni muhimu katika kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Mkutano huo unafanyikawakati ambapo waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na maafisa wengine wakuu wanapanga kujibu shambulio la kombora la Iran la Oktoba mosi.
Soma Zaidi: Israel yashambulia vikali Hezbollah mjini Beirut
Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia wakimbizi wa Kipalestina limetoa wito wa kupatikana suluhu angalau ya muda mfupi ili kuruhusu watu kuondoka kutoka kwenye maeneo ya kaskazini mwa Gaza.
Maafisa wa afya katika eneo hilo wameeleza kwamba hawana vifaa vya kutibu wagonjwa waliojeruhiwa katika mashambulizi ya Israel yaliyodumu kwa wiki tatu mfululizo katika eneo hilo.
Amjad Al-Shawa, mkuu, Mtandao wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Palestina ameelezea juu ya hali ngumu ya upatikanaji wa chakula na dawa katika eno la kaskazini mwa Gaza.
Philippe Lazzarini, mkuu wa shirika la misaada la UNRWA, amesema hali ya kibinadamu imefikia pabaya. Amesema operesheni za UNRWA zinakaribia kusimama katika Ukanda wa Gaza kwa sababu ya hali inayozidi kuwa ngumu.
Licha ya miito mingi ya kimataifa kwa Israel kuruhusu uingizaji wa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, jeshi la Israel linaendelea kuweka vikwazo vikali.
Huku hayo yakiendelea jeshi la Israel leo limetoa wito kwa wakaazi wa kitongoji cha kusini mwa Beirut kuhama kabla ya operesheni za kijeshi kuanza kuwalenga wapiganaji na vituo vya Hezbollah katika eneo hilo.
Msemaji wa jeshi la Israel Avichay Adraee ameandika kwa lugha ya Kiarabu kwenye jukwaa la X akisema “Kwa usalama wako na usalama wa familia yako, lazima uondoke kwenye majengo yatakayolengwa mara moja”.
Wizara ya afya ya Lebanon imesema watu 13, akiwemo mtoto, wameuawa katika shambulizi la Israel karibu na hospitali ya umma ya Chuo Kikuu cha Rafik Hariri, iliyoko kusini mwa Beirut. Mashambulizi hayo ya anga yamesababisha uharibifu mkubwa kwenye hospitali hiyo kubwa kabisa nchini Lebanon.
Hezbollah kwa upande wake imeendeleza msururu wa mashambulizi ya roketi kuelekea katikati mwa Israel, imesema imeshambulia kwa roketi maeneo mawili katika vitongoji vya kibiashara mjini Tel Aviv na kituo cha wanamaji karibu na mji wa kaskazini wa Haifa.
Soma Zaidi: Israel yaendelea kuishambulia Lebanon
Vita vya Gaza na Lebanon vimevutia makundi mengine yenye silaha yenye mafungamano na Iran, ya Yemen, Syria na Iraq.
Vyanzo: AFP/RTRE