Mahakama yasikiliza kesi ya kupinga kuenguliwa kwa Gachagua – DW – 22.10.2024

Mahakama ya kuu ya Kenya imeendelea kuisikiliza rufaa ya naibu wa rais wa Kenya aliyeondolewa madarakani Rigathi Gachagua, kupinga mchakato uliomuengua kwenye kiti chake wiki iliyopita. Kesi hiyo inaendelea wakati Rais Wiliam Ruto  akisema mahakama inayoisikiliza haina mamlaka ya kufanya hivyo.

Kesi hiyo inasikilizwa baada ya Mahakama Kuu ya Nairobi kusimamisha mchakato wa kuondolewa madarakani kwa Gachagua. Maamuzi hayo yalifanyika muda mfupi baada ya bunge kumuidhinisha Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki kuchukua nafasi ya naibu wa Rais.

Soma zaidi: Rigathi Gachagua asema ulinzi wake umeondolewa

 Rufaa hiyo inaendelea wakati Rais William Ruto akiweka pingamizi na kusema Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza rufaa hiyo na inapaswa kuiachia suala hilo Mahakama ya Juu kwa kuwa inahusu suala la kikatiba. Rigathi Gachagua aliyehudhuria mahakamani Jumanne aling’olewa mamlakani na baraza la Seneti Ijumaa alikokuwa akikabiliwa na shutuma 11 ikiwemo kuchochea migawanyiko ya kikabila. Mwenyewe amekanusha tuhuma zote na timu yake ya sheria imekata rufaa ikidai kuwa mchakato wa kumuengua umeharakishwa na si wa haki.

Gachagua alilazwa hospitali baada ya kupatwa na maumivu ya kifua muda mfupi kabla ya kutoa ushahidi mbele ya baraza la Seneti, lakini baraza hilo lilikataa kuuchelewesha mchakato huo.

Gachagua amwita Ruto “mtu katili”

Baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali, alimtuhumu vikali Ruto na kumwita “mtu katili” huku akidai kuwa amewahi kutishiwa maisha kipindi cha nyuma ikiwa ni pamoja na kuwekewa sumu kwenye chakula. Naibu huyo wa rais aliyeenguliwa alisema pia kuwa ameondolewa ulinzi na wafanyakazi wake wote wamepewa likizo ya lazima. 

William Ruto
Rais wa Kenya William RutoPicha: LEON NEAL/POOL/AFP via Getty Images

Hii ni mara ya kwanza kiongozi wa ngazi yake kung’atuliwa kwa namna hiyo katika kile kinachoonekana kuwa mzozo wa wazi kati ya Gachagua na Rais Ruto. Wachambuzi wanadhani kuwa kuondolewa kwa Gachagua huenda kukamsaidia Ruto  kuimarisha utawala waake ambao ulitikiswa na maandamano ya kuipinga serikali ambayo ndiyo makubwa zaidi katika miaka miwili ya utawala wake.   

Rais William Ruto aliyemchagua Gachagua kama mgombea mwenza katika uchaguzi wa Agosti 2022, bado hajazungumza lolote kuhusu kung’olewa mamlakani kwa msaidizi wake. 

Siku ya Jumapili Ruto alitoa wito wa kulindwa kwa maadili ya kitaifa na kanuni za utawala kila siku, bila ya kuihusisha moja kwa moja kauli hiyo na naibu wake  aliyeenguliwa.

Gachagua alimsaidia Ruto kupata uungwaji mkono katika eneo muhimu la Mlima Kenya  katika uchaguzi uliopita, hatua iliyopelekea ushindi katika mchuano huo mkali dhidi ya mpinzani wake na mwanasiasa mkongwe Raila Odinga.

 

 

Related Posts