Kufikia mchana wa Jumanne (Oktoba 22), tayari Rais Putin alishamkaribisha na kufanya mazungumzo ya pande mbili na Waziri Mkuu Narendra Modi wa India na Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini.
Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Rais Putin amesema uhusiano baina ya India na Urusi unazidi kuimarika kila uchao na kwamba kwa pamoja serikali za mataifa hayo zinao uwezo wa kuzikabili changamoto kwenye siasa za kilimwengu.
“Mahusiano ya Urusi na India yana tabia ya ushirikiano mkubwa wa kimkakati na yanaendelea kuimarika kwa kasi. Tunaupokea na kuukaribisha uamuzi wako wa kufungua Ofisi ya Ubalozi wa India mjini Kazan. Utanuzi wa nafasi ya kidiplomasia ya India nchini Urusi utachangia zaidi kwenye maendeleo ya pande zetu mbili.” Alisema Putin.
Soma zaidi: Putin mwenyeji wa mkutano wa kilele wa BRICS
Kwa upande wake, Modi, ambaye hii ni mara ya pili kuizuru Urusi kwa nia ya kusaka makubaliano ya kusitisha vita vya Ukraine, alitumia fursa ya mazungumzo yake ya leo na Putin kurejelea msimamo wake huo.
“Kuhusiana na mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine, tumekuwa na mawasiliano ya kudumu baina yetu na tunaamini matatizo haya yanapaswa kumalizwa kwa njia ya amani. Tunaunga mkono kikamilifu hatua za kufikia amani na utangamano haraka iwezekanavyo. Kwenye juhudi zetu, tunaweka kipaumbele chetu kwenye ubinaadamu, na tuko tayari kutoa msaada wowote utaohitajika.” Alisema Modi.
Modi aliitembelea Ukraine mnamo mwezi Agosti na alikuwa Urusi mwezi Julai mwaka huu kuzitaka pande hizo mbili zikae kwenye meza ya mazungumzo, huku India ikibeba jukumu la kuwa mpatanishi mkuu.
Ramaphosa amsifia Putin kama rafiki wa kweli
Kwa upande wake, Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini, ambaye nchi yake ni miongoni mwa waanzilishi wa jumuiya ya BRICS, alimuambia mwenyeji wake, Rais Putin, kwamba nchi yake inathamini sana kile alichokiita “mahusiano tunu” baina ya mataifa yao mawili. Rais huyo wa Afrika Kusini alisema Putin ni rafiki na mshirika wa kweli kwa Afrika Kusini tangu zama za vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Rais Xi Jinping wa China, Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ni miongoni mwa viongozi wakubwa wa ulimwengu ambao wanahudhuria mkutano huu wa siku tatu wa jumuiya inayokuwa kwa kasi ya BRICS, ambayo inasaka kujitambulisha kama mbadala wa mfumo na madhubuti wa kimataifa kando ya ulimwengu unaotawaliwa na mataifa ya Magharibi.
Soma zaidi: Ukraine yamlaumu Guterres kukubali mwaliko wa kuhudhuria mkutano wa kilele wa BRICS
Mkutano huo ambao wengi wanasema unajenga taswira ya jinsi mataifa ya Magharibi yalivyoshindwa kwenye juhudi zao za kuitenga Urusi baada ya uvamizi wake dhidi Ukraine, unatarajiwa kupitisha maazimio muhimu sana juu ya ushirikiano wa kifedha utakaoukwepa mfumo unaotawaliwa na Marekani.