M23 wanapambana na Wazalendo kuudhibiti mji wa Kalembe – DW – 23.10.2024

Mji huo uliotangazwa kukombolewa  hapo Jumatatu  na makundi ya vijana hao wazalendo baada ya siku moja kuchukuliwa na M23,  sasa ni kitovu cha mapigano kati ya pande zote mbili. Kulingana na vyanzo vya ndani, leo Jumatano wapiganaji wa kundi la M23 wamezidisha mashambulizi yao katikati mwa mji huo.  

Tangu mapema alfajiri ya leo, wapiganaji wa kundi la M23 walizishambulia kwa mizinga ngome za  vijana wanaojiita wazalendo katikati mwa mji huo wa Kalembe. Taarifa zinasema kuwa, wapiganaji wa makundi hayo ya vijana wanaoungwa mkono na jeshi la serikali ya Kongo,  yalijikuta yamezingirwa na waasi wa M23 na ghafla kuanza kurushiana mabomu. Hata hivyo, mashirika ya kiraia yaliyothibitisha mapigano haya yanayoendelea hadi mchana huu, yamedai kuwa maelfu wa raia wanaokimbia bado wanahangaika. 

Umuhimu wa mji wa Kalembe katika taifa la Kongo

DR Kongo | M23 Rebellen
Mmoja wa waasi wa M23 akonekana anondoka kwenye eneo la Kibumba la mkoa wa Kivu Kaskazini wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Desemba 23, 2022.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Kalembe ni mji muhimu sana wenye wakazi zaidi ya 40,000 unaopatikana katika eneo la Masisi, Rutshuru na Walikale ambapo M23 wanapigania kuingia. Hapo juzi Jumatatu jeshi la serikali ya Kongo kupitia msemaji wake Sylvin Ekenge lilitangaza udhibiti wa Kalembe na vikosi vya wazalendo siku moja tu baada ya M23 kuchukua udhibiti wa mji huo. 

Ongezeko la machafuko katika mji huo, limewatia wasiwasi mkubwa raia pamoja na wanasiasa mkoani Kivu Kaskazini ambao wametaka uwajibikaji wa serikali ya Kongo  katika vita hivi.

Mji huo unatoa ufikiaji rahisi katika wilaya ya walikale, eneo lenye utajiri mkubwa wa madini, na ambapo kuna migodi mikubwa ya dhahabu  ambayo iko chini ya udhibiti wa jeshi tiifu kwa serikal. Hadi tunapoandaa ripoti hii, pande zote mbili zinapigana kwenye kijiji kidogo  cha Katahandwa ambacho ni cha mwisho kabla  ya kuingia Kalembe karibu kilometa 140 magharibi mwa mji wa Goma vimeeleza vyanzo vya kiraia.

Soma zaidi:Mapigano mapya yazuka kati ya M23 na Wazalendo Mashariki mwa DRC

Mapigano haya mapya, yanaendelea kukwamisha mchakato wa usitishaji mapigano eneo hili kama ilivyotakiwa na viongozi wa kikanda mwanzoni wa mwezi wa Agosti chini ya upatanishi wa nchi ya Angola.  

 

 

 

 

 

Related Posts