Ni lazima kupima vyakula vya Mifugo-Dkt. Makondo

Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imewataka wazalishaji na wauzaji wa vyakula vya Mifugo kupima ubora vya vyakula wanavyovizalisha ili kujiradhisha kama vinakidhi ubora unaotakiwa kwa lengo la kulinda afya za mifugo pamoja wa watumiaji wa mazao ya mifugo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo Oktoba 22, 2024 alipokuwa akifanya ukaguzi wa vyakula vya Mifugo kwa wazalishaji na wauzaji wa vyakula hivyo Mkoa wa Pwani (Kibaha, Mlandizi na Kisalawe) oktoba 21 na 22, 2024 kujiridhisha kama taratibu zilizowekwa na wizara zinafuatwa ikiwemo uhuishaji na ukataji vibari vya uzalishaji na uuzaji wa vyakula vya mifugo sambamba na kuhakiki ubora wa vyakula hivyo.

“Vyakula vyote vya mifugo vinavyozalishwa vinasimamiwa na sheria ya nyanda za marisho, ni lazima vyakula vyote viwe vimepimwa ili kujihakikishia viwango vilivyokubalika kwa matumizi ya Mifugo. Mnatakiwa kujiridhisha kama chakula kimehakikiwa ubora na kinafaa kwa matumizi. Tunapita kukagua pamoja na kutoa elimu. kwa wale tutakaowabaini wanavunja sharia, tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria. Tusifanye kazi kwa mazoea, tunatakiwa kulinda afya za mifugo na walaji.” Alisema Dkt. Makondo.

Kwa upande wake Mkaguzi wa vyakula vya Mifugo Wilaya ya Kisalawe Mkoa wa Pwani Dkt. Kimboka Juma amewataka wauzaji na wazalishaji wa vyakula vya Mifugo kuweka chapa kwenye mifuko ya vyakula, kuzingatia usafi wa mazingira ya kuuzia vyakula hivyo ili viendelee kubaki na ubora pamoja na kuajili wauzaji waliosomea vyakula vya Mifugo.

Meneja wa Kiwanda cha Animal Care Company ltd kilichopo Mlandizi mkoa wa Pwani Bw. Aijeno Ngogo ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kwa kuendelea kuwatembelea, kuwakagua na kuwapa ushauri wa vitu vinavyotakiwa kufuatwa na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa ustawi wa Mifugo.

Mkaguzi wa vyakula vya Mifugo Wilaya ya Kisalawe Mkoa wa Pwani Dkt. Kimboka Juma akikagua pamoja na kuchukua sampuli ya vyakula vya Mifugo kwa ajili ya kwenda kupima kutoka kwa muuzaji wa vyakula hivyo Bi. Sarah Juma (kulia) alipotembelea duka kwake Kiluvya Oktoba 22, 2024 ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa viwanda na maduka ya vyakula vya Mifugo.
Mkaguzi wa vyakula vya Mifugo Wilaya ya Kisalawe Mkoa wa Pwani Dkt. Kimboka Juma akikagua pamoja na kuchukua sampuli ya vyakula vya Mifugo kwa ajili ya kwenda kupima kutoka kwa muuzaji wa vyakula hivyo Bi. Sarah Juma (kulia) alipotembelea duka kwake Kiluvya Oktoba 22, 2024 ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa viwanda na maduka ya vyakula vya Mifugo.
Mkuu wa kitengo cha Sayansi ya Wanyama wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Scholastica Doto (katikati) akichukua taarifa za vyakula vya Mifugo pamoja na kuchukua sampuli za vyakula hivyo kutoka kwa Muuzaji Bi. Rehema Abdalah (kulia) alipotembelea duka kwake Kiluvya Wilaya ya Kisalawe Oktoba 22, 2024 ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa viwanda na maduka ya vyakula vya Mifugo.
Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo (kulia mbele) akipata maelezo kuhusiana na uzalishwaji wa vyakula vya Mifugo kutoka kwa Meneja wa kiwanda cha Animal Care Company LTD Bw. Aijeno Ngogo (mbele kushoto) kilichopo Mlandizi Mkoa wa Pwani alipotembelea kiwanda hicho Oktoba 21, 2024 ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa viwanda na maduka ya vyakula vya Mifugo.

Mkurugenzi wa Huduma za Uchunguzi kutoka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Zacharia Makondo (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Backbone Bw. Gong Feng kuhusiana na Maabara ndogo za uchunguzi wa vyakula vya Mifugo za kiwanda hicho kilichopo kibaha Mkoa wa Pwani alipotembelea kiwanda hicho Oktoba 21, 2024 ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa viwanda na maduka ya vyakula vya Mifugo.

Related Posts