Nishati safi ya kupikia yapigiwa chapuo Jumuiya ya Madola

 

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, ametoa rai kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, kuwa mstari wa mbele katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kutimiza mpango wa Jumuiya hiyo wa nishati endelevu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Apia, Samoa … (endelea).

Waziri Kombo ameyasema hayo leo wakati wa majadiliano ya ajenda ya Jumuiya ya Madola ya Nishati Endelevu (The Commonwealth Sustainable Energy Transitions Agenda -CSETA), yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM), unaoendelea jijini Apia, kisiwani Samoa.

Kombo anayemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye mkutano wa CHOGM, amesema nchi zinazoendelea Tanzania ikiwamo, zinakabiliwa na changamoto ya bei kubwa na mazoea ya watu kutumia kuni au mkaa.
Amezialika nchi za jumuiya hiyo kushirikiana na Tanzania kuwekeza kwenye sekta mbalimbali, ikiwamo nishati safi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Dk. Arjoon Suddhoo, amesema mjadala huo utaisaidia Jumuiya ya Madola, kuona maeneo ya kushirikiana ili kukuza matumizi ya nishati endelevu.

Amesema eneo muhimu ni kujenga uwezo na kubadilishana teknolojia, ili kuharakisha kufikia Ajenda ya Nishati endelevu kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Mbali ya nishati safi, mkutano utamchagua Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola na washiriki watajadili uwekezaji, kutafuta suluhu ya pamoja kwa ajili ya maendeleo endelevu, mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia, uchumi, demokrasia na amani.

Mkutano huu pia utaibua changamoto na matarajio ya wanachama, huku Tanzania kama moja ya wanachama 56 wa Jumuiya ya Madola ikiwa miongoni mwa wale watakaonufaika katika sekta za uwekezaji, mabadiliko ya tabianchi, uchumi stahimilivu na kubadilishana ujuzi.

Aidha, Waziri Kombo ameshiriki mkutano wa Jukwaa la Biashara la Jumuiya ya Madola (CBF), uliowakutanisha viongozi wa ngazi za juu wa Jumuiya ya Madola akiwemo, Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Jumuiya ya Madola, Lord Marland, Waziri Mkuu wa Samoa, Fiamē Naomi Mataʻafa, viongozi wa serikali na wafanyabiashara.

Mkutano wa CBF umejikita kutafuta suluhu za pamoja za kiuchumi zenye kulinda mazingira kupitia biashara ikiwemo uchumi wa buluu na uchumi wa kijani.

Aidha, ameshiriki mkutano wa masuala ya michezo ya Jumuiya ya Madola uliowakutanisha viongozi, maofisa, mashirika ya michezo na wanariadha, ambao wamejadili dhima ya michezo katika kufikia malengo ya kijamii, kiuchumi na kiafya kwa watu wa rika zote, kwenye nchi wanachama.

Mkutano wa 49 wa CHOGM, unafanyika jijini Apia, nchini Samoa kuanzia tarehe 21 hadi 26 Oktoba 2024, ukiongozwa na kaulimbiu ya ‘Ustahimilivu katika kufikia malengo ya pamoja ya kimaendeleo.’

About The Author

Related Posts