TATIZO la kutokukumbukwa katika ajiri kwa Watu wenye ulemavu wa macho kutoka na kutokufuatwa kwa sheria ya Ajira kwa Watu wenye ulemavu imetajwa kuwa ni tatizo kubwa linaloikumba jamii.
Hayo yameeleza na Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye ulemavu wa macho Tanzania, Habiba Salum wakati akizungumza katika kongamano la fimbo nyeupe kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 tangu kuazishwa kwa Chama hicho lililofanyika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro.
Alisema kuwa, wapo walemavu wa kutokuona ambao wamesoma na wanavyeti vyao lakini ajira hawana hivyo nioombe serikali iangalie wakati inapofanya usaili iangalie kundi hili.
“Tatizo linalotukabili kwa wingi sisi walemavu wa macho ni ajira katika kada yetu wapo wasomi wengi na wanavyeti vyao lakini hawajapata ajira, nilikuwa naiomba serikali wakati huu inafanya usahili kwa ajili ya kuwapata wafanyakazi waiangalie kada hii” Alisema Habiba.
Na kuongeza ” Kama sikosei ipo sheria inayoelekeza asilimia tatu ya ajira ni kwa watu wenye ulemavu ingawa serikali inajitahidi ila bado katika sekta binafsi jambo hili halizingatiwi kama wangetimiza tatizo la ajira lisingekuwa kubwa”.
Aidha Mwenyekiti huyo, alisema kuwa bado jamii inakabiliwa na tatizo la unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu kwa kuwafungia ndani na kuwanyima huduma za kijamii.
Wakati huo huo Mwenyekiti huyo, alisema kuwa Kongamano hilo watalitumia kuwahamasisha wananchi kutambua watu wenye ulemavu wa macho ni wa aina gani na wanamahitaji ya aina gani lakini pia madereva waweze kutambua fimbo nyeupe inamaana gani.
Akifungua Kongamani hilo, Mratibu wa Chama cha Wasioona Tanzania(TLB) Kizito Wambura aliwaonya watu ambao wamekuwa wakiwatumia watu wenye ulemavu wa macho kujipatia kipato kuacha tabia hiyo kwani ni kosa kwa mujibu wa sheria na yeyote atakayebainika kufanya hivyo atafikishwa mahakamani.
Wambura alisema kuwa, Kongamani hilo pia litatumika kutoa maoni yao kwa ajili ya kuhuisha sera ya Taifa ya watu wenye ulemavu wa macho ambayo sera hiyo ilitungwa mwaka 2004 na ni muda mrefu umepita hivyo inahitaji kufanyiwa mapitio.
“Hili haliwezi kufanyika na Watendaji pekee linahitaji kukusanya maoni kutoka kwa wadau ambao moja ya wadau hao ni Chama cha Wasioona Tanzania lakini tutakwenda kuangalia maswala ya ujumuishwaji wa miundombinu mbalimbali ya kutolea huduma ili kuhakikisha jamii hiyo haikabiliwi na changamoto wakati wa upatikanaji wa huduma” Alisema Wambura.
Nao baadhi ya Washiriki wa Kongamano hilo akiwemo Mwalimu Mussa Mashauri alisema kuwa, mtazo wa jamii kwa watu wenye ulemavu wa wasioona sio mzuri huku pia suala la umaskini likitajwa kama kikwazo kwa jamii ya Watu wenye ulemavu wa macho.