Wadau wa Elimu kutoka ofisi ya elimu ya jimbo la Gwangju nchini Korea Kusini ambao ni viongozi na walimu kutoka taasisi ya utafiti ya elimu na habari (GERIS) wametembelea shule ya msingi Mkombozi Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe na kupongeza jitihada za wanafunzi wa shule hiyo namna wanavyoweza kuitumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kujifunza na kutengeneza vifaa mbalimbali wakiwa masomoni baada ya walimu wao kunufaika na masomo ya matumizi ya TEHAMA nchini Korea Kusini.
Ujumbe huo wa watu nane kutoka nchini Korea Kusini ambao ni walimu wa fani mbalimbali umeongozwa na Bw.Park Laejin ambaye ni Mkurugenzi wa masuala ya TEHAMA kutoka taasisi ya Elimu na utafiti wa teknolojia ya Habari Gwangju waliombatana na baadhi ya viongozi Kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) umeshuhudia namna wanafunzi kutoka shule ya Mkombozi wakionyesha umahiri wa kuitumia TEHAMA vyema kujifunzia hali ambayo imeelezwa itasaidia kuwaongezea kufanya vizuri zaidi kielimu wakati ulimwengu wa sasa unakimbizana na teknolojia.
Akizungumza juu ya umahiri wa wanafunzi hao kwenye matumizi ya teknolojia, Bw. Park Laejin ameishukuru serikali ya Tanzania na Korea Kusini kuwa na mashirikiano ambayo yanasaidia kuleta matokeo chanya kwa sasa katika matumizi ya TEHAMA kwenye shule za msingi na sekondari nchini Tanzania.
“Haya mafunzo tunayotoa kuhusu TEHAMA ningependa yawe mafunzo yatakayosaidia pia jamii nzima ya watu wa mkoa wa Njombe, natutatumia wasaa wakati tupo Njombe kuwapa tena mafunzo walimu waliopata mafunzo nchini Korea Kusini ili wapate ujuzi zaidi,” amesema Rasjin.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka ambaye amefanya mazungumzo ofisini kwake na ujumbe huo na wenyeji wao kutoka TET amewashukuru kwa kufanya ziara mkoani hapo na kupongeza mashirikiano yaliyopo baina ya nchi mbili katika kusaidia kwenye mafunzo ya TEHAMA.
“Ni jambo zuri katika mashirikiano kwenye mahusiano ya kitaaluma baina ya mji wa Njombe na Gwangju na wakirudi nchini kwao wafikishe salamu zetu kutoka kwa mimi kiongozi wa mkoa wa Njombe, tunashukuru na kutambua mchango mkubwa ambao wao wamefanya kwenye kusaidia TEHAMA kwenye eneo letu,” amesema Mtaka.
Awali, Mkurugenzi wa mafunzo ya Mitaala wa TET,Dk. Fika Mwakabungu amesema ujumbe huo umefika mkoani hapo kutokana na ushirikiano uliopo baina ya ofisi mbili za elimu kutoka Tanzania na Korea Kusini katika maeneo makuu matatu ikiwemo kushirikiana kwenye miundombinu ya TEHAMA ambayo inawezesha katika ufundishaji na ujifunzaji, kutoa mafunzo endelevu kwa walimu waliopo kazini namna bora ya kutumia TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji..
“Eneo la tatu ni kuwawezesha wanafunzi kuwamotisha katika kutumia TEHAMA na teknolojia saidizi, ambapo nje ya TEHAMA wanafunzi wameweza kutumia betri mbalimbali na kuweza kuunganisha saketi za umeme kupata umeme na umeme rahisi,” amesema Fika.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Habari na Machapisho (TET) Bw. Kwangu Zabrone akizungumzia manufaa ya ujumbe huo mkoani Njombe katika sekta ya elimu, amesema kuwa anamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa na kuamini kwamba elimu ya Tanzania inaweza ikaboreka kwa matumizi sahihi ya TEHAMA.