WHI yatunukiwa Tuzo ya Nyumba za Gharama Nafuu Barani Afrika

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Watumishi Housing Investment (WHI) imetunukiwa tuzo ya heshima ya ‘Nyumba za Gharama Nafuu Zaidi Afrika,’ iliyotolewa na Taasisi ya Mikopo ya Nyumba Afrika (AUHF), inayotambuliwa na Umoja wa Afrika.

Afisa Mtendaji Mkuu wa WHI, Dk. Fred Msemwa, akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati wa mkutano huo.

Tuzo hiyo ilitolewa kwenye Mkutano Mkuu wa AUHF wa mwaka 2024, uliofanyika hivi karibuni visiwani Zanzibar, ambapo WHI iliibuka kidedea miongoni mwa taasisi mbalimbali zinazoshughulika na sekta ya makazi kutoka mataifa kadhaa barani Afrika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 23, 2024, Afisa Mtendaji Mkuu wa WHI, Dk. Fred Msemwa alisema tuzo hiyo ni ishara ya kutambua juhudi za WHI katika kuwezesha umiliki wa nyumba kwa watu wa kipato cha chini na kati nchini Tanzania.

“Tuzo hii inatambua juhudi za WHI katika kutoa suluhisho la malipo nafuu ya nyumba, ikiwemo mpango wa malipo endelevu bila riba wakati wa ujenzi na utaratibu wa mpangaji kuwa mnunuzi, ambao vimetajwa kama sababu kuu za ushindi wetu,” alisema Dk. Msemwa.

Aliongeza kuwa mpango huu umekuwa msaada mkubwa kwa Watanzania wengi wanaotamani kumiliki nyumba, huku WHI ikiuza nyumba zake kwa bei nafuu zaidi ikilinganishwa na soko. “Nyumba za WHI zinauzwa kwa bei nafuu hadi asilimia 10 chini ya bei ya soko, na bei ya kuanzia ni Shilingi milioni 38,” alifafanua.

Dk. Msemwa alieleza kuwa tuzo hiyo pia inakuja katika kipindi muhimu, wakati WHI ikisherehekea miaka 10 ya ubunifu na uongozi katika sekta ya makazi. WHI imekuwa taasisi ya kwanza nchini Tanzania na Afrika Mashariki kutunukiwa tuzo hii ya heshima.

“Tuzo za AUHF zinatambua michango thabiti katika kuendeleza sekta ya makazi barani Afrika. Ushindi wa WHI unatokana na utekelezaji wake wa kipekee wa miradi ya nyumba za gharama nafuu, ikilenga zaidi watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii,” alisema Dk. Msemwa.

Aliendelea kusema kuwa AUHF, shirika linalounganisha wadau wa makazi barani Afrika kwa zaidi ya miaka 40, linawezesha washirika wake kuendeleza suluhisho la makazi ya bei nafuu. “Ahadi ya WHI ya kupunguza gharama za makazi na kutoa njia mbadala za malipo imeonekana kuwa hatua kubwa kuelekea kufikia maono haya,” alisema.

Tuzo hiyo pia inathibitisha dhamira ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, katika kuwawezesha wananchi kupata makazi nafuu.

WHI ni taasisi ya umma chini ya Ofisi ya Rais, UTUMISHI, inayosimamia maendeleo ya milki na mifuko ya uwekezaji wa pamoja, ikiwa na jukumu la kusimamia Mfuko wa Nyumba na Mfuko wa Faida Fund.

Related Posts