BASHUNGWA AMBANA MKANDARASI KASI NDOGO UJENZI WA BARABARA YA NYAMWAGE – UTETE

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa hajaridhishwa na usimamizi na kasi ya ujenzi wa wa barabara ya Nyamwage – Utete (km 33.7) kwa kiwango cha lami na kumuagiza Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Pwani, Eng. Baraka Mwambage kumsimamia Mkandarasi China Railway Seventh Group (CRSG) akamilishe kuleta Wataalam pamoja na Mitambo itakayomwezesha kutekeleza mradi kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba.

Bashungwa ametoa agizo hilo leo Oktoba 24, 2024 Wilayani Rufiji Mkoani Pwani wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo na kutoridhishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo ambapo hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 7.

“Meneja wa TANROADS hakikisha unamsimamia Mkandarasi kama mikataba inavyosema, nitarudi hapa kukagua nataka nione timu yote ya wataalam wakiwa wamejipanga pamoja na vifaa vya kazi vikiwa site, hiyo siku ukiwa hujasimamia haya narudi na wewe Dodoma”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaiwezesha Wizara ya Ujenzi fedha za ujenzi wa barabara hiyo ambapo Mkandarasi hadai malipo kwa sasa kwahiyo hana sababu yoyote ya msingi ya kutoongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo.

Aidha, Bashungwa amemtaka Mkandarasi CRSG kujitathimini katika miradi yote anayoitekeleza kwa kuwa amekuwa akisua sua katika baadhi ya miradi ya ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja katika Mikoa ya Mara, Katavi, Ruvuma, Dar es Salaam na Pwani.

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameidhinisha kuanza kwa maandalizi ya ujenzi wa barabara mpya km 354 inayotoka Chalinze – Magindu- Bwawa la Mwalimu Nyerere – Utete.

Nae, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Pwani Eng. Baraka Mwambage ameahidi kumsimamia mkandarasi huyo ili aweze kuongeza kasi ya kufanya kazi wastani wa asilimia 8 kwa mwezi ambapo sasa anafanya kazi wastani wa asilimia 2.1 kwa mwezi.





Related Posts