Honda Yazindua Toleo Jipya la Honda ACE 150

Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Honda Ukanda wa Afrika Kusini, Hideki Shinjo (kushoto) akiwaongoza baadhi ya wageni wa meza kuu kuzindua rasmi pikipiki aina ya ACE 150 Jinjini Dar es Salaam leo Oktoba 24,2024 Wengine kutoka Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama Cha Maderevena na Wamiliki wa Pikipiki Dar es Salaam, Mike Massawe ASP Rosemary Kitwala, Meneja wa Honda Tanzania Frank Mushi na Msaidizi wa Mkurugenzi wa Honda Afrika Kusini, Hiroki yoshinaka.

Na Mwandishi wetu Michuzi TV 

WAENDESHA pikipiki nchini Tanzania sasa wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kampuni ya Honda Motors leo kuzindua toleo la ACE 150 lililoboreshwa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa Honda Motors Kusini mwa Afrika, Hideki Shinjo amesema wanaona fahari kuzindua toleo jipya la Honda ACE 150 nchini Tanzania kwa kuwa ni mojawapo ya masoko zaidi ya kimkakati kwa Honda Motors, ambayo imemaliza tu kuadhimisha miaka 76 tangu kuanzishwa kwake 1948..

“Tanzania ni mojawapo ya masoko yetu ya kimkakati, hivyo tumejitolea kusambaza bidhaa zenye ubora wa juu kwa bei nafuu inayowaridhisha wateja," alisema.

Aidha, alidokeza kwamba mafanikio ya Honda Motors nchini Tanzania ni matokeo ya kuendelea kuwekeza katika ubunifu ili kuhakikisha huduma zetu zinakidhi matarajio ya mteja. 

“Tumejitolea kuunda bidhaa za ubunifu kama hii mpya ya ACE 150 ambayo si tu inaongeza wepesi wa watu kusafiri, lakini pia inanufaisha jamii kwani pikipiki ni chanzo cha mapato na kwa sasa ni moja ya vyanzo vikubwa vya kutengeneza ajira katika sekta ya umma na ya kibinafsi,” alisisitiza.

Meneja wa Kampuni ya Honda Tanzania, Frank Mushi, alisema ACE 150 ni ya kipekee na inayofaa kwa watumiaji kwani imeboreshwa ikilinganishwa na ACE 125 na 110 ambazo watu wengi wameizoea.

“ACE 150 mpya inakuja na vipengele vingi vipya na vya kusisimua kama vile sehemu ya USB kwa kuchaji simu za kiganjani, geji ya mafuta, rimu ya magurudumu, kifuniko cha taa ya mbele na helmeti 2,”alieleza, na kuongeza kwamba wateja watakuwa na uchaguzi mpana wa rangi, zikiwemo nyeusi, ambayo ni ya kwanza kuzalishwa kwani nyekundu na bluu zilikuwepo hapo awali.

Alibainisha pia kwamba ACE 150 mpya ina injini yenye nguvu zaidi na ni imara zaidi barabarani, hivyo kuna uhakika wa usalama wa mwendesha pikipiki na abiria.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi na ya umma kwa vile walipata nafasi ya kuuliza maswali na pia kujaribu toleo jipya la ACE 150.

Related Posts