Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla akizungumza na wataalamu kutoka Mali wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano na Posta ya Mali (AMRTP)
na Wakala wa Usimamizi wa Mfuko wa Upatikanaji wa Huduma za Mawasiliano kwa Wote (AGEFAU) waliokuja nchini kwa ajili ya kujifunza na kubadilishana uzoefu katika tasinia ya Mawasiliano na TEHAMA na
kufika Wizarani hapo leo Oktoba 24, 2024 jijini Dodoma.
Matukio katika picha wakati wa kikao kazi cha Wataalamu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na wataalamu kutoka nchi
ya Mali waliofika Wizarani hapo leo Oktoba 24, 2024 jijini Dodoma kwa cha kubadilishana uzoefu kuhusu uratibu na usimamizi wa tasnia ya Mawasiliano na TEHAMA.
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amepokea na kuikaribisha timu ya wataalamu kutoka nchi ya Mali kwa ajili ya kujifunza kutoka katika Serikali ya Tanzania namna kuratibu na kusimamia masuala yote
yanayogusa tasnia ya mawasiliano na TEHAMA.
Akizungumza na ujumbe huo leo Oktoba 24, 2024 Wizarani Dodoma, Bw. Abdulla amesema Wizara hiyo na taasisi zake wapo tayari kutoa ushirikiano kwa kuwa kuna maeneo mengi ambayo nchi ya Mali inaweza kujifunza Tanzania yakiwemo masuala ya akili mnemba (AI).
“Kama nchi kupitia Wizara hii tuna mafanikio na mipango mingi ambayo ipo kwenye hatua za utekelezaji ikiwa ni pamoja na kujenga chuo kikubwa cha umahiri cha TEHAMA na Kituo kikubwa zaidi cha kuhifadhia Data hivyo mnakaribishwa sana kujifunza kutoka kwetu”, amesisitiza Abdulla.
Naye Bw. Ibrahima Abdoulaye Kone, kiongozi wa wataalamu hao wa Mali amesema kuwa Mali ina mengi ya kujifunza kutoka Tanzania hasa katika muundo wa kitaasisi, umoja na ushirikiano uliopo kwa taasisi zinazoshughulikia masuala ya mawasiliano na TEHAMA.
Amesema kuwa, nchini Mali, uratibu na usimamizi wa taasisi zinazojihusisha na masuala ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA haupo katika Wizara moja kama ilivyo kwa Tanzania hivyo kusababisha baadhi
ya maeneo kushindwa kuratibiwa vema.
Ameongeza kuwa asilimia 99 ya wananchi wa Mali wanamiliki simu janja ambapo bei ya kifurushi cha data kwa GB moja ni sawa ni dola za kimarekani mbili sawa na shilingi 5500 fedha za kitanzania.
Wataalamu hao kutoka Mali wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano na Posta ya Mali (AMRTP) na Wakala wa Usimamizi wa Mfuko wa Upatikanaji wa Huduma za Mawasiliano kwa Wote (AGEFAU) waapo nchini kuanzia Oktoba 21 hadi 26, 2024 kwa ajili ya kujifunza na
kubadilishana uzoefu na Wizara; Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF); Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); na kampuni simu ya Airtel.