Katika juhudi za kuwasaidia vijana kujitegemea kiuchumi Mkoani Kilimanjaro,wilaya ya Hai,kundi la vijana hasa hasa wanawake limepata fursa ya kipekee ya kushiriki katika mafunzo ya ufugaji wa kuku yaliyoratibiwa na shirika la SHUJAAZ.
Akizungumza wakati wa Mafunzo hayo leo tarehe 24 Oktoba,2024 Meneja wa Mradi wa “BINTI SHUJAAZ” Bw.Lucky Komba amesema kuwa mafunzo haya yamelenga kutoa elimu kuhusu mbinu bora za ufugaji wa kuku,matunzo sahihi ya kuku,lishe bora, afya na matibabu ya kuku, pamoja na masoko na faida za biashara ya kuku.
Sambamba na hilo Bw.Komba ameeleza kuwa mradi huo una lengo pia la kuelewa changamoto ambazo vijana wa kike wazopitia na zinazowafanya washindwe kanya vizuri katika swala zima la ufugaji wa kuku.
Aidha Afisa Mifugo na uvuvi Wilaya ya Hai Bw.Fratern Mtika amewaasa vijana wa kike wa Kitanzania ambao hawana kazi,waanze kufikiria fursa ya ufugaji wa kuku wa kisasa kwani inatija,watumie vizuri asilimia 10 ya mkopo wa vijana ili kujikwamua kiuchumi.
Hata hivyo amewataka vijana wa kike kuzingatia kanuni za ufugaji bora ili kupata matokeo mazuri. Aidha,wazingatie uandaaji mzuri wa bajeti ya mradi, kutunza rekodi za shughuli za ufugaji, na kujenga mahusiano mazuri na wafugaji wenzao na wateja.
Mmoja kati ya vijana wakike alieshiriki mafunzo hayo Aisha Mbaga amesema kupitia mafunzo haya,wameongeza ujuzi wao,na nimatumaini yao watakuwa na uwezo wa kujitegemea kiuchumi na kuwa chachu ya maendeleo katika jamii yao,aidha wamepata motisha ya kufanya kazi kwa bidii na kujikita katika biashara ya ufugaji wa kuku kama njia ya kujipatia kipato,huku wakichangia katika kupunguza umaskini katika jamii yao.
Vijana wa Wilaya ya Hai wamelishukuru Jukwaa la SHUJAAZ kwa kuwapa fursa hiyo ya kipekee na kuwapa ujuzi na maarifa muhimu ya kujikwamua kiuchumi,na kuhaidi kutumia vyema mafunzo waliyopokea na kuendelea kukuza uchumi wao kwa manufaa yao binafsi na ya jamii yao kwa ujumla.