WAZIRI SILAA AZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 436.4 MKALAMA

 

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, leo Oktoba 24, 2024, amezindua mradi wa maji na Zahanati yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 436.4 katika wilaya ya Mkalama, mkoani Singida.

Mradi wa maji uliozinduliwa katika kijiji cha Nkalakala, umegharimu shilingi milioni 348.9 na unapunguza changamoto waliyokuwa nayo wananchi ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Meneja wa RUWASA wilaya ya Mkalama, Mhandisi Christopher Saguda, alisema tanki hilo lina uwezo wa lita 90,000 litaweza kuhudumia vituo 12 vya kuchotea maji, huku ujenzi wake ukiwa umekamilika kwa asilimia 100.

Mradi mwingine uliozinduliwa na Waziri Silaa ni zahanati ya Igonia iliyopo kijiji cha Mtogo Mwili uliogharimu shilingi Milioni 87.4 ambao ulianza kutekelezwa kwa michango ya wananchi kabla ya Serikali kuendeleza ujenzi wake.

Zahanati hiyo itahudumia vijiji vya Igonia, Ikungu, na Mtamba, ikinufaisha wananchi 1,408 kulingana na sensa ya 2022. Huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma za wagonjwa wa nje na uzazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Silaa amekagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi (VETA) katika kijiji cha Mwando, ambao umefikia asilimia 30 na unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.4.

Kwa nyakati tofauti wananchi wa wilaya ya Mkalama wameeleza shukrani zao kwa Rais Samia kwa kutenga fedha kwa ajili ya miradi hiyo ya maendeleo.

Related Posts