Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Msimu wa kumi na tano wa Shindano la kusaka vipaji, Bongo Star Search African (BSSA), umewatangaza rasmi majaji na watangazaji watakaoongoza mashindano haya yanayopanuka kwa mara ya kwanza hadi nchi jirani.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu wa BSSA, Madam Rita Paulsen, alifichua majina ya majaji watakaoshiriki msimu huu, huku Prodyuza mahiri wa muziki S2kizzy Zombi akiwa mmoja wao.
Madam Rita alisema, “Mashindano haya yatashirikisha kikosi kazi cha majaji waliobobea watakaoongoza msimu huu wa kihistoria. Jaji Mkuu nitakuwa mimi, Madam Ritha, nikiwa na Master J (Johakim Kimario), Prodyuza S2kizzy Zombi, na Salama Jabir kutoka Tanzania, pamoja na majaji wawili wa kimataifa kutoka Kenya na Uganda – Sanaipei Tande na Lilian Mbabazi.”
Madam Rita pia alikaribisha Prodyuza S2kizzy kwenye familia ya BSSA, akisema, “Napenda kukukaribisha katika familia ya Bongo Star Search African. Naam, naamini utakuwa na mchango mkubwa katika kutafuta vipaji vipya.”
Aidha, kwa upande wa ushereheshaji, Idris Sultan na Meena Ally watakuwa watangazaji wa msimu huu, wakiongoza shindano kutoka mwanzo hadi tamati. Madam Rita aliwapa moyo washiriki kwa kusema, “Washiriki wetu, huu ni wakati wenu. Hii ni nafasi ya kipekee inayoweza kubadilisha maisha yenu. Ushiriki wenu ni safari ya kujifunza, kukua, na kufikia malengo makubwa.”
Prodyuza S2kizzy Zombi, ambaye pia ni miongoni mwa majaji wapya, alieleza furaha yake kwa kujiunga na BSSA, akisema ilikuwa ndoto yake ya siku nyingi kufanya kazi na shindano hilo. “Kwa miaka yangu yote niliyofanya kazi na wasanii wakubwa wa ndani na nje ya Tanzania, nina imani tutafanya mambo ya kushangaza Afrika,” alisema Zombi.
Bongo Star Search African msimu huu unalenga kuwa zaidi ya shindano la vipaji – ni safari ya kufungua milango kwa wasanii chipukizi kutoka Afrika Mashariki na Kati, na kutoa jukwaa la kimataifa kwa wanamuziki wenye ndoto na bidii.