Mtanzania achaguliwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia

Na Benny Mwaipaja, Washington D.C

Benki ya Dunia imemchagua Mtanzania, Dk. Zarau Kibwe, kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki hiyo atakayesimamia Kanda Namba Moja ya Afrika inayojumuisha nchi 22 ikiwemo Tanzania, nafasi ambayo Tanzania imewahi kuihudumu miaka 54 iliyopita.

Uamuzi wa Dk. Kibwe kuipewa nafasi hiyo nyeti katika Taasisi hiyo kubwa ya Fedha Duniani, umetangazwa katika Mkutano wa Mwaka wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Benki ya Dunia, uliofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani ambapo mikutano ya mwaka ya Shirika la Fedha Duniani IMF na Benki ya Dunia inafanyika.

Kabla ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo, Dk. Kibwe, alihudumu katika Ofisi hiyo ya Bodi kama Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Mshauri na Mshauri Mwandamizi kwa zaidi ya miaka saba, tangu mwaka 2017.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba (kulia), akimpongeza Dk. Zarau Kibwe, kwa kuchaguliwa na Benki ya Dunia kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Benki hiyo atakayesimamia Kanda Namba Moja ya Afrika.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF, Washington D.C-Marekani)

Akizungumza Jijini Washington D.C, baada ya kutangazwa kuchukua nafasi hiyo, amesema kuwa ataitumia nafasi hiyo kusimamia uendeshaji wa Benki na taasisi zake pamoja na kutetea maslahi ya nchi katika Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia pamoja na maslahi ya Kanda ya Afrika anayoisimamia ili kukuza maendeleo na uchumi wa nchi hizo.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali katika Mkutano huo uliomtangaza Dk. Kibwe kuchukua nafasi hiyo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, anayeongoza Ujumbe wa Tanzania katika mikutano hiyo, amesema kuwa hayo ni matokeo ya juhudi za Dk. Samia Suluhu Hassan, anavyoifungua nchi na kukuza Diplomasia ya Kimataifa.

Dk. Nchemba amempongeza Dk. Kibwe kwa kupata nafasi hiyo na kwamba kutokana na umahili wake katika masuala ya uchumi na fedha, pamoja na uzoefu wake wa muda mrefu katika Ofisi hiyo, anaamini kuwa maslahi ya nchi yataendelea kulindwa ipasavyo kwa manufaa ya watanzania.

Dk. Kibwe ni mchumi wa kitanzania ambaye hivi karibuni amechaguliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia kwa Kanda Namba Moja ya Afrika inayojumuisha nchi za Botswana, Burundi, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Gambia, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Shelisheli, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda, Zambia, na Zimbabwe.

Kabla ya kujiunga na Ofisi ya Bodi, Dk Kibwe alihudumu kama Mchumi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania ambapo katika kipindi cha miaka 15 ya kazi yake, amehudumu katika Serikali ya Jamhuri wa Muungano katika nafasi mbalimbali ikiwemo ya Mchambuzi Mwanadamizi wa Sera (Ofisi ya Rais – Tume ya Mipango), Mhadhiri Msaidizi (Chuo Kikuu Dodoma), Afisa Forodha Msaidizi (Mamlaka ya Mapato Tanzania), na Mhadhiri Msaidizi (Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere).

Dk. Kibwe ana Shahada ya Uzamivu (Ph.D.) katika Uchumi wa Maendeleo, Shahada ya Uzamili (MA) katika Uchumi wa Maendeleo, na Shahada ya Umahiri katika Sera za Umma, zote kutoka Taasisi ya Taifa ya Mafunzo ya Sera (GRIPS) huko Tokyo, Japani. Alipata Shahada yake ya Kwanza ya Sayansi katika Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe kilichopo Morogoro, Tanzania.

Related Posts