Usaili wa wasanii Bongo Star Search African kuanzia Arusha Novemba 9

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shindano la kusaka vipaji la Bongo Star Search African (BSSA) limepanga kuanza rasmi usaili wa wasanii nchini Tanzania, ambapo usaili wa awali utaanza Mkoani Arusha Novemba 9 hadi 10 katika ukumbi wa SG Resort, Mianzini.

Akizungumzia ratiba ya usaili, Mkurugenzi wa Benchmark, Rita Paulsen maarufu kama Madam Rita, alifafanua kuwa usaili utaendelea katika mikoa mbalimbali nchini na nchi jirani.

Madam Rita alisema, “Usaili utaanza Arusha Novemba 9 hadi 10, 2024, katika SG Resort Mianzini, kisha tutahamia Mwanza Novemba 16 hadi 17 kwenye hoteli ya La Kairo. Usaili utaendelea Kampala Novemba 23 hadi 24, Nairobi Novemba 30 hadi Desemba 1 katika Little Theater, Babati Desemba 6 hadi 7 Olympic Lounge, na mwisho Dar es Salaam Desemba 13 hadi 15, 2024, kwenye Makumbusho ya Taifa.”

Pia aliwashukuru wadhamini wa shindano hilo kwa mchango wao mkubwa katika kukuza tasnia ya burudani nchini na kufanikisha upanuzi wa mpango huo hadi nje ya mipaka ya Tanzania. “Tunatoa shukrani za dhati kwa wadhamini wetu na washirika wa Bongo Star Search. Ushirikiano wenu umetufanya kufikia malengo ya kupanua wigo na kufikia zaidi ya mipaka ya Tanzania,” alisema Madam Rita.

Mashindano haya yataonyeshwa moja kwa moja kupitia vituo vya televisheni vya Star Times: St Swahili Channel kwa Tanzania, Makula TV kwa Uganda, na St Swahili chaneli 160 & 400 kwa Nairobi, ili kuwapa watazamaji fursa ya kufuatilia shindano hili kubwa kwa karibu.

Related Posts