Na Linda Akyoo -Moshi
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Oktoba 25, 2024 amewaasa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu kwani wanahaki sawa na watoto wengine na niwatanzania pia.
Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa ameyasema hayo mkoani Kilimanjaro ambapo anamwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Fimbo Nyeupe na Miaka 60 ya Chama cha Wasioona Tanzania (TLB).
Siki ya Kimataifa ya Fimbo Nyeupe huadhimishwa kila Oktoba 15 kwa lengo la Kuelimisha jamii kuhusu haki na uwezo wa watu wenye ulemavu wa kuona, Kutambua umuhimu wa fimbo nyeupe katika kusaidia watu wenye ulemavu wa kuona kusafiri kwa usalama na uhuru na hatimaye kufikia malengo yao.
Aidha Mhe.Majaliwa amehamasisha ujumuishaji wa watu wenye ulemavu wa kuona katika jamii na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika elimu, ajira, na huduma zote nyingine.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Mhe.Nurdin Babu ameishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira vijana na wenye ulemavu kwa kuchagua mkoa wa Kilimanjaro kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya siku ya fimbo nyeupe duniani na miaka 60 ya Chama cha Wasioona Tanzania.
Sambamba na hilo amewahasa watu wanaoishi na ulemavu kujitokeza na kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ifikapo tarehe 27 Oktoba,2024 ili kuchaguwa kiongozi wamtakae.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Upatikanaji wa Teknolojia Saidizi na Fikivu ni Mkombozi kwa Uchumi Endelevu kwa Mtanzania asiyeona.”