BENKI YA DUNIA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MRADI WA UJENZI MAJENGO 16 CHUO KIKUU CHA MWALIMU JULIUS NYERERE CHA KILIMO NA TEKNOLOJIA

Benki ya Dunia imeridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa majengo 16 ya Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kampasi Kuu Butiama kupitia mradi wa Elimu ya juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Akizungumza Oktoba 25,2024 Mkoani Mara Kiongozi kutoka Timu ya Benki hiyo wanaotembelea maeneo ya mradi wa HEET Prof. Roberta Malee amesema kuwa wamefurahishwa na kujivunia kwa namna mradi unavyotekelezwa kwa ubora na ufanisi.

Malee ameongeza kuwa wanaona namna Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inavyoweka jitihada
katika kusimamia mradi kwa kufuata viwango vya ubora vilivyowekwa na Benki ya Dunia katika Mradi huo.

” Tunaona bidii katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kufuata ubora unaohitajika na Benki ya Dunia tunafurahi sana kwa kinachoendelea hapa” amesisitiza Malee

Naye Mtaalamu Mwandamizi wa Elimu kutoka Benki ya Dunia Nkahiga Kaboko ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayanyna Teknolojia kwa kuwa na sera nzuri ya kuendeleza Elimu ya Juu nchini na kuisimamia

Ameongeza kuwa kinachoonekana MJNUAT ni moja ya Juhudi za Serikali kuhakikisha elimu ya Juu inachangia katika uchumi wa nchini.

“Kama tunavyojua Duniani kote maendeleo ya nchi yanachangiwa kiasi kikubwa pia na elimu ya juu hivyo unapokuwa na miundombinu inayotoa fursa kwa watu kupata elimu ya juu bora una uhakika wa kupata wataalamu wazuri ambao watachangia katika sekta mbalimbali na kutengeneza ajira kwa njia ya kuanzisha makampuni pamoja na kufanya tafiti mbalimbali “

Related Posts