Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa rai kwa Viongozi wa Dini kote nchini, kutumia majukwaa yao kusaidia Serikali kutoa elimu sahihi ya kuepuka na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kama Mpox, Kipindupindu na Marbug.
Dkt. Mollel ameyasema hayo Oktoba 26, 2024 wakati akimuwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama kwenye Mkutano wa Waziri wa Afya na viongozi wa Dini kuhusu tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko na suala la Bima ya Afya kwa Wote.
Amesema viongozi hao wana wajibu wa kiroho wa kusaidia kuhakikisha wanailinda jamii na maradhi yanayoepukika kwa kutumia majukwaa yao ya ibada.
“Tunazungumza nanyi kwa niaba ya waumini, viongozi wa dini kote nchini isaidieni Serikali kutoa elimu sahihi ya kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama Mpox, Kipindupindu na Marbug,” amesema Dkt. Mollel.
Ameongeza kuwa jitihada za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendeleza jitihada za afua mtambuka ili kuhakikisha nchi inabaki salama.
“Wakati tukifuatilia wasilisho tumeona ramani ya Tanzania ikiwa nyeupe lakini wenzetu wanao tuzunguka wameshapata visa vya baadhi ya magonjwa ya mlipuko, sasa niwaombe muemde mkazungumze na wanajamii ili ramani ya Tanzania izidi kubaki nyeupe,” amefafanua Dkt. Mollel
Naye katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu akihitimisha mkutano huo amesema ipo haja ya pande hizo mbili kuendelea kufanya kazi kwa pamoja ili wananchi ambao niwaumini kwenye nyumba za ibada kuwa salama na kuendelea na majukumu yao.
“Tumekubaliana tunatoka hapa tukiwa na nia moja, tunaenda kuwahimiza waumini wetu lakini pia na sisi wenyewe kwa usafi ndio kila kitu, baadhi ya mila na desturi zetu zinazokuwa hatarishi tuziepuke na sisi tuwajibike na kuhakikisha tunaendelea kuwa salama na mwisho wa siku nchi yetu kwa ujumla itakuwa salama,” amesema Dkt. Jingu.
Kwa upande wao wawakilishi wa viongozi wa dini wameipongeza Serikali kwa kutumia majukwaa ya dini kuendelea kufikisha elimu ya afya kwa umma na kuahidi kwenda kuwahimiza waumini dhidi ya magonjwa hatarishi ya mlipuko.