TAASISI ZA UMMA ZITUMIE MIFUMO RASMI YA SERIKALI MTANDAO: MH.MACHANO

Na Mwandishi wetu Zanzibar

Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na Watendaji wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ), wametembelea Makao Makuu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mtumba jijini Dodoma.

Ujumbe huo, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati Mh.Machano Othman Said, umetembelea e-GA ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika kuendeleza eneo la Serikali Mtandao Tanzania Bara na Visiwani.

Sambamba na wajumbe hao, ugeni huo uliongozana na Mhe. Ali Suleiman Ameir – Waziri wa Nchi Afisi ya Raisi Ikulu, Zanzibar pamoja na Ndg. Saleh Juma Mussa – Katibu Mkuu – Afisi ya Rais, Ikulu Zanzibar.
Katika ziara hiyo kamati ilipata taarifa ya utekelezaji wa hafua mbalimbali za Serikali Mtandao kutoka kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba.

Baada ya kupokea taarifa hiyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh.Machano Othman Said ametoa wito kwa Taasisi za Umma nchini kutumia mifumo rasmi ya TEHAMA ili kuendeleza utawala bora,kudhibiti mapato ya serikali na kulinda usalama wa nchi katika zama hizi za sayansi na Teknolojia.

Mh. Machano amesema kuwa, Serikali zote mbili zina utayari wa mageuzi ya TEHAMA katika uendeshaji wa shughuli za serikali za kila siku katika kuwahudumia Watanzania.

” Kila tukiwasikia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Dkt.Hussein Mwinyi wamekuwa vinara katika kuleta mapinduzi ya kidijiti na kuonesha umuhimu wa TEHAMA katika utendaji, hivyo tusisitize Taasisi zote kutumia mifumo ya TEHAMA katika utendaji kazi wao wa kila siku” ameeleza Mh.Machano.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa e-GA Mhandisi Benedict Ndomba, ameahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanziba (eGAZ) ili kuhakikisha Serikali Mtandao inaimarika kote Bara na Visiwani.






Related Posts