Na Mwamvua Mwinyi,Mafia
SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itaunda Timu Maalum itakayoshughulikia kupata suluhu ya kudumu ya vivuko vya TNS Songosongo na Mv Kilindoni ambavyo havifanyikazi kwa takriban siku 18 sasa.
Akikagua kivuko cha Songosongo Oktoba 26,2024 wakati wa ziara yake maalum Mkoani Pwani, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa alieleza ,Serikali kwa kushirikiana na Jeshi la wananchi JWTZ yenye kivuko cha Songosongo na Wakala wa ufundi na umeme (TEMESA) inafanya jitihada ya kutatua hali hiyo.
Serikali ipo kazini, na kupitia timu hii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani itafanya jitihada za haraka za kurudisha huduma za vivuko viwili vya MV Kilidoni na Meli ya TNS Songosongo ili kuwaondolea adha wana Mafia ya kukosa usafiri wa Vivukoā€¯, amesisitiza Bashungwa.
Alieleza, kwasasa njia inayotumika kufika kisiwa cha Mafia kirahisi ni njia ya anga suala ambalo linakwamisha wananchi wa hali ya chini pamoja na kushindwa kusafirisha baadhi ya mitambo,vifaa mbalimbali vya miradi.
Bashungwa alieleza kuwa Mkakati wa Serikali ni kuongeza kivuko kingine ili kusaidia wakati wa dharura kwa kutoa huduma kwa wananchi pindi kivuko kingine kinapopata hitilafu.
Vilevile Bashungwa alisisitiza ,mpango wa Serikali kuhakikisha inaboresha barabara ya Bungu hadi Nyamisati na maeneo korofi yanapitika.
“Hii itasaidia wakati vivuko vikiwa vimetengemaa iweze kufungamana na barabara inayopitika kwa urahisi japo kwa kiwango cha changalawe kwa kuanzia.
Kadhalika, Waziri huyo alieleza kuna haja ya kuwa na mkakati maalum wa kuendelea kutangaza Mafia ili kuinua sekta ya utalii.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema Ofisi yake inaendelea kuongea na Wawekezaji wa Sekta binafsi watakaoweza kufanya uwekezaji wa huduma ya Usafiri na Hoteli ili kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma hizo ambazo zitaendelea kufungua uchumi wa Wilaya ya Mafia.
Awali akitoa taarifa ya wilaya Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo alisema ,hali ya usafiri ni ngumu inakwamisha usafiri Mafia -Nyamisati.
Alieleza kuwa, njia itayotumika ni ya anga lakini pia wanashughulikia uwepo wa kufungwa taa kwenye bajeti ijayo.
Mkazi wa Kilindoni Hafsa Nassoro na Juma Hassan walisema ,kilio cha usafiri wa uhakika ni mtihani mkubwa kwa wana Mafia.
Nassoro alisema ,hadi sasa ni siku ya 18 tangu tarehe 10, oktoba 2024 wasafiri wa Mafia na Nyamisati wamekwama kutokana na kukwama kwa usafiri.
Kutokana na matengenezo ya mara kwa mara ya vivuko vilivyopo,Wizara na TEMESA ipo kwenye mchakato wa kuongeza kivuko kipya ili kupunguza adha ya ongezeko la wasafiri wa pande zote mbili Nyamisati na Mafia itakayokuwa na uwezo wa kubeba Tani 120 na watu 500,chenye gharama zaidi ya Bilioni 9.