Wakuu wa Polisi Afrika Mashariki Waahidi kushirikiana kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Wakuu wa polisi kutoka nchi sita za Afrika Mashariki na Kati wameahidi kushirikiana kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni ambao unaonekana kushika kasi katika ukanda huu.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Ramadhani Kingai, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Camilius Wambura, katika mkutano wa nane wa wakuu wa polisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Oktoba 25, 2024.

Kingai amesema Tanzania inaendelea kudhibiti uhalifu wa mtandaoni kutokana na operesheni mbalimbali zinazofanyika mara kwa mara. “Hatuna matukio makubwa ya mtandao zaidi ya wale wanaobahatisha. Hii ni kutokana na operesheni zinazosababisha wahalifu kukamatwa na kufikishwa mahakamani,” alisema Kingai.

Ushirikiano wa Kanda kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka

Kingai ameongeza kuwa mkutano huo umejikita katika kujadili masuala ya kiusalama, hususani uhalifu unaovuka mipaka, ili kuwezesha nchi hizo kushirikishana taarifa kwa ufanisi.

“Kuna matukio ambayo huwezi kuyatatua peke yako mpaka uende kwa mwenzako kuvuka mipaka. Kwa kushirikiana, tutaweza kuwafanya wananchi wetu kuwa na uelewa zaidi na kuimarisha usalama,” alieleza.

Kingai amesisitiza kuwa uhalifu wa mtandaoni ni mpya katika kanda hii, na kuna haja ya Watanzania kujifunza mbinu mpya za kupambana nao. “Kwa nchi za Afrika Mashariki, changamoto ni uhalifu wa mitandaoni na viashiria vya ugaidi. Hata hivyo, juhudi za viongozi wa nchi na vyombo vya ulinzi na usalama zinawaweka wahalifu katika nafasi ngumu ya kufanikisha uhalifu huu,” alifafanua.

Tanzania yaendelea kuwa kivutio cha mikutano ya kiusalama

Kamishna Kingai aliishukuru Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo, akisema kuwa hatua hiyo inadhihirisha kuwa nchi inaendelea kuwa salama.

Aidha, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Thomas Jal Thomas kutoka Sudan Kusini, alisisitiza umuhimu wa kushirikiana katika kukabiliana na makosa yanayovuka mipaka, akisema mkutano huo utaangazia mbinu za kusaidia waathirika wa uhalifu wa mtandaoni.

“Kinachojadiliwa hapa kitasaidia kuhakikisha tunadhibiti matukio haya na kuweka mazingira salama kwa nchi zetu zote za Afrika Mashariki,” alisema Thomas.

Wakuu hao wa polisi wameahidi kuimarisha juhudi za pamoja na kuendelea kushirikishana taarifa muhimu, kuimarisha usalama wa kanda na kuwezesha wananchi kuendelea kuishi kwa amani na usalama.

Related Posts