WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amempgia simu na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala kufika mara moja katika Kisiwa cha Mafia kupiga kambi kusimamia matengenezo ya Kivuko cha MV Kilindoni na kuhakikisha hawatoki mpaka huduma ya usafiri wa kivuko kati ya Nyamisati – Mafia itakaporejea na kutoa huduma kwa wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mafia, Pwani … (endelea).
Bashungwa ametoa maelekezo hayo wakati akitoa ufafanuzi kwa Wananchi kuhusu kusimama na kukosekana kwa huduma ya usafiri wa vivuko katika Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani ambapo Wananchi wamelalamikia kukosa huduma ya vivuko na kupelekea kutumia vyombo vya usafiri visivyo salama na uhakika pamoja na kushindwa kusafirisha bidhaa na huduma nyingine.
“Katibu Mkuu kufika kesho kutwa wewe au Naibu Katibu Mkuu uje hapa Mafia uambatane na Mtendaji Mkuu wa TEMESA mpige kambi muone kilio na uchungu wa wananchi wa Mafia wanaoupata, Msitoke hapa mpaka kivuko kianze kutoa huduma kwa wananchi. Kivuko kikianza kufanya kazi ndio mnipigie simu niweze kuwaruhusu kutoka huku Mafia,” amesisitiza Bashungwa.