Wajapan wamepiga kura katika uchaguzi wenye ushindani mkali ambao haujawahi kuonekana kwa miaka,huku waziri mkuu mpya Shigeru Ishiba na chama chake chenye nguvu cha Liberal Democratic kikikabiliwa na uwezekano wa kupata matokeo mabaya kabisa tangu mwaka 2009.
Uchunguzi wa maoni nchini humo unaonesha chama hicho cha kihafidhina pamoja na washirika wake katika muungano wanakabiliwa na kitisho cha kuporomoka na kushindwa kupata wingi wa viti bungeni,hali ambayo huenda ikawa pigo kubwa kwa waziri mkuu Ishiba.
Waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 67,aliyewahi pia kuwa waziri wa ulinzi aliitisha uchaguzi wa mapema mara baada ya kuingia madarakani kufuatia kuchaguliwa kwake kwa wingi mdogo wa kura kukiongoza chama hicho cha LDP,ambacho kimeitawala Japan kwa takriban miongo saba iliyopita.
Kero za wapiga kura
Hata hivyo wapiga kura katika taifa hilo la nne kwa nguvu za kiuchumi duniani wamekasirishwa na hali ya kupanda kwa bei na athari zilizosababishwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha za kampeini yaliyofanywa na chama cha LDP,kashfa iliyopelekea kumporomosha waziri mkuu aliyekuwepo Fumio Kishida.
Waziri mkuu wa sasa Ishiba ameahidi kuinua hali ya maeneo ya vijijini na kushughulikia suala la dharura la kuporomoka kwa idadi ya watu nchini Japan,kwa kuanzisha hatua zitakazovutia mazingira ya kukuza familia ikiwa ni pamoja na mpangilio mzuri wa masaa ya kufanya kazi.
Lakini kiongozi huyo ameonesha kutokuwa tayari kuunga mkono masuala kadhaa ikiwemo kuruhusu wanandowa kuwa na majina tofauti.Sambamba na hilo kwenye baraza lake la mawaziri aliteuwa mawaziri wawili tu wanawake.
Maoni ya wapiga kura
Tafiti nyingi za maoni ya wapiga kura zilizoendeshwa na vyombo vya habari nchini Japan zimeonesha kwamba LDP na washirika wake wadogo katika serikali ya muungano,Komeito huenda wakahangaika kupata idadi ya viti 233 inayohitajika kulidhibiti bunge.Soma pia: Waziri Mkuu wa Japan Kishida hatagombea tena uenyekiti wa chama chake
Lengo kubwa la Ishiba ni kufikia kiunzi hicho na hatua ya kushindwa kufikia lengo hilo itamaanisha nafasi yake katika chama cha LDP itakabiliwa na changamoto, na hilo litamaanisha kwamba atabidi kutafuta washirika wengine wa kuunda nao serikali au kuongoza serikali isiyokuwa na wingi.
Siku ya Jumamosi,waziri mkuu Ishiba akizungumza kwenye mkutano wa hadhara alisema wanataka mwanzo mpya,wa chama chenye haki,na ukweli na kwahivyo anawaomba ridhaa wapiga kura kukipa nafasi chama chake ya kuongoza.
Vyombo vya habari ndani ya Japan vinakisia kwamba Ishiba huenda akakabiliwa hata na uwezekano wa kujiuzulu mara moja, na hivyo kumfanya kuwa waziri mkuu wa kwanza kushikilia nafasi hiyo kwa muda mfupi zaidi katika historia ya nchi hiyo ya baada ya vita.