WAZIRI wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameweka mawe ya msingi na kuzindua miradi minne ya maendeleo yenye jumla ya shilingi bilioni 1.793 katika Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mpanda, Katavi … (endelea).
Katika siku ya pili ya ziara yake Mkoani humo, leo tarehe 27 Oktoba 2024, Waziri Mbarawa amefanya ukaguzi ukarabati wa Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ambao umegharimu kiasi cha shilingi milioni 900 pamoja na kuweka jiwe la msingi ujenzi wa shule mpya ya Msingi ya Kawajense ambayo ujenzi wake umekamilika 100% kwa gharama ya shilingi milioni 561.
Pia ameweka jiwe la msingi ujenzi wa vyumba 5 vya madarasa na matundu 6 ya vyoo katika shule ya Sekondari Magamba ambayo ujenzi wake umegharimu Sh. 144 milioni.
Vile vile amekagua na kuweka jiwe la msingi mradi wa ukarabati wa vyumba 6 vya madarasa, Ofisi moja ya Waalimu na matundu 9 ya vyoo katika shule ya msingi Kashaulili uliogharimu Sh. 188 milioni.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara eneo la Kazima Ringini Manispaa ya Mpanda; Waziri Mbarawa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya huku akitoa wito kwa Wananchi kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kunufaisha vizazi vijavyo.