RAIS SAMIA ANAFANYA MAMBO MAKUBWA YA MAENDELEO KWA WATANZANIA_MKUCHIKA

Na Mwandishiii wetu, Morogoro

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum), Mhe. Kapt. George Mkuchika, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya mambo makubwa kwa maendeleo ya Watanzania kwa kuboresha sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, afya na barabara.

Mkuchika amesema hayo Oktoba 26, 2024 akiwa mkoani Morogoro katika ziara ya kikazi ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

“Katika Shule ya Sekondari Kingolwira Rais Samia ametoa zaidi ya Shilingi Milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manne na matundu nane ya vyoo kwa wanafunzi hasa wa kidato cha kwanza mwaka 2024”, ameeleza Mkuchika.

Amesema kuwa shule hiyo pia imepokea kiasi cha Shilingi Millioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 pamoja na utengenezaji wa vitanda 40.

Aidha Waziri Mkuchika amesisitiza wananchi waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024.

“Nawapongeza wananchi wa Morogoro kwa sababu kitaifa mkoa huu umekuwa wa tatu kwa kuandikisha watu wengi katika Daftari la Wapigakura wa Serikali za Mitaa, kama umejiandikisha na hautajitokeza kupiga kura utakuwa umepoteza muda wako wa kujiandikisha”, ameeleza Mkuchika.

Waziri Mkuchika anaendelea na ziara ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imepeleka fedha ili kuboresha maisha ya Watanzania.

Related Posts