Matokeo hayo yametiliwa shaka pia waangalizi, Umoja UIaya na Marekani wakipendekeza uchunguzi wa haraka.
Kwa mujibu wa matokeo ya awali ya tume ya uchaguzi, chama tawala cha Georgian Dream kilishinda kwa 54.8% ya kura wakati muungano wa vyama vinne vya upinzani vinavyoupigia upatu Umoja wa Ulaya, ukiibuka na asilimia 37.58%.
Soma pia: Upinzani nchini Georgia waitisha maandamano kupinga matokeo ya uchaguzi wa bunge
Akisimama pamoja na viongozi wa upinzani, Bi Zourabichvili aliwahimiza raia wa Georgia kuandamana leo Jumatatu katika barabara kuu ya mji wa Tbilisi kupinga kile alichokiita uchakachuaji wa matokeo na wizi wa kura zao.
Ameongeza kusema kwamba nchi yake imekuwa muhanga wa kile alichokitaja kuwa “operesheni maalum ya Urusi” iliyolenga kuiondoa kwenye muelekeo wa Ulaya.
“Siutambui uchaguzi huu. Uchaguzi huu hauwezi kutambuliwa kwa sababu kufanya hivyo itakuwa sawa na kutambua kuingia kwa Urusi hapa, itakuwa sawa na Georgia kujisalimisha kwa Urusi.”
Ikulu ya Kremlin kupitia msemaji wake Dmitry Peskov imekanusha madai ya kuhusika katika uchaguzi wa Georgia na akisema kwamba shutuma hizo hazina uthibitisho kabisa.
Ukosoaji zaidi
Waangalizi kutoka mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali ya Georgia pamoja na Chama cha Wanasheria Vijana wa Georgia vile vile wamelalamikia ukiukaji mkubwa katika uchaguzi na kuripoti visa vingi vya watu binafsi kupiga kura zaidi ya mara moja.
Vyombo vya habari vya Georgia vimenukuu Waziri Mkuu Irakli Kobakhidze akisema kuwa upinzani ulikuwa unajaribu kupindua “utaratibu wa kikatiba” na kwamba serikali yake bado inaendeleza dhamira yake ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Wakati Marekani na Umoja wa Ulaya wakionyesha wasiwasi kuhusu madai ya udanganyifu na kutoa wito wa uchunguzi wa haraka, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban alikaidi wito huo na anatarajia kufanya ziara mjini Tbilisi ili kudhihirisha ushirikiano na uungaji mkono wake kwa chama cha Georgian Dream.
Hata hivyo mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesisitiza kuwa Orban hauwakilishi umoja huo katika chochote atakachokisema, na kwamba rais huyo wa mzunguko wa Umoja wa Ulaya hana mamlaka juu ya sera ya kigeni.
Uhusiano wa Georgia na Urusi
Kwa miaka mingi, Georgia imekuwa moja ya nchi zinazoungwa mkono na nchi za Magharibi kuondoka kutoka katika ushaswishi wa Moscow, huku kura za maoni zikionyesha Wageorgia wengi hawapendi Urusi lijihusiha katika masuala ya nchi yao.
Urusi iliishinda Georgia katika vita vyao vifupi dhidi ya waasi jimbo la Ossetia Kusini mnamo 2008.
Matokeo ya uchaguzi wa Jumamosi katika taifa hilo la zamani la Kisovieti yanaleta changamoto kwa matarajio ya Umoja Ulaya kuongeza wanachama wake hasa kutoka mataifa ya zamani ya Kisovieti.