Korti yabariki Tamisemi isimamie uchaguzi

 

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Dar es Salaam leo, Jumatatu Oktoba 28.2024 imetupilia mbali shauri lililokuwa limefunguliwa Mahakamani hapo na Watanzania watatu (3) ambao ni Bob Chacha Wangwe, Bubelwa Kaiza na Dk. Ananilea Nkya dhidi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambapo Watanzania hao walikuwa wanapinga Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI kuratibu na kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa 2024. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Shauri hilo ambalo lilitajwa Mahakamani hapo leo kwa ajili ya kutolewa maamuzi kufuatia mapingamizi matatu (3) yaliyokuwa yamewekwa na Jamhuri, ambapo kwa mujibu wa Jaji David Ngunyale aliyelikuwa anasikiliza pingamizi hilo ameyataja mapingamizi hayo kutokuwa na nguvu ya moja kwa moja ya kuishawishi Mahakama kufanya maamuzi hatua iliyoilazimu Mahakama kujielekeza kwenye shauri la msingi

Amesema katika kuliangalia shauri hilo, Mahakama ilianza kuangalia endapo mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI ana mamlaka ya kuandaa kanuni zinazomuongoza kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa

Amesema Mahakama iliangali kama kuna matumizi mabaya ya mamlaka kutoka kwa Waziri huyo, ambapo awali waleta maombi waliishinikiza Mahakama kwa kueleza kwamba mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Waziri hakuwa na mamlaka ya kisheria ya kumuwezesha kutunga kanuni za uchaguzi huo

Katika ushawishi wao, upande wa waleta maombi waliileza Mahakama hiyo kuwa mjibu maombi wa kwanza anakosa sifa kwa kuwa yeye ni mwanasiasa, Waziri, na kwamba moja kwa moja ana maslahi ya uchaguzi kutokana na kwamba anatoka kwenye chama tawala hivyo haikubaliki kuona mtu wa aina yake anakuwa msimamizi wa uchaguzi

Imeelezwa kuwa, hoja hizo zilipingwa vikali na upande wa Jamhuri ambao katika utetezi wake walisema kuwa Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI hawezi kusababisha mgongano wa maslahi kwa kuwa anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na si utashi wake, jambo ambalo limekubalika na Mahakama

Aidha, Jaji Ngunyale amesema viko vifungu kadhaa vya kisherie vinavyompa mamlaka Waziri kutengeneza kanuni hizo za uchaguzi, na kwamba suala la kudai kuwa ataendesha zoezi hilo na kusababisha mgongano wa maslahi kutokana na kwamba anatoka kwenye chama tawala ni la kihisia, lisilokuwa na uthibitisho kamili na kwamba Mahakama hiyo haiwezi kufanya maamuzi ya kihisia ikizingatiwa kuwa kwa sasa Waziri kuna vifungu vinamruhusu kufanya hivyo ikiwemo kifungu cha 201(a) cha mamlaka za serikali za mitaa

Ameendelea kufafanua kuwa, kama tatizo linaanzia kwenye sheria hilo ni jambo lingine, na kwamba anaamini ndio maana mwananchi aitwaye Wallace Mayunga ameamua kufungua shauri la Kikatiba akihoji suala hilo huku akitambua kwa sasa Waziri analindwa na sheria katika majukumu yake

Kuhusu hoja ya kwamba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwa ndio chombo kinachopaswa kusimamia uchaguzi huo, Mahakama imeeleza kukubaliana na hoja za upande wa Jamhuri kuwa INEC itakuwa huru kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa endapo itatungwa sheria rasmi na Bunge itakayoipa mamlaka hayo, lakini kwa sasa hakuna sheria hiyo badala yake sheria iliyotungwa na Bunge mwanzoni mwa mwaka huu ilieleza kuwa INEC itatekeleza jukumu hilo kwa kufuata sheria itakayotungwa na Bungea, sheria ambayo haijatungwa, na kwamba si kweli kuwa sheria mpya inapotungwa basi sheria ya awali inafutika moja kwa moja badala yake upo utaratibu uliowekwa nchini wa kisheria wa jinsi kufutwa kwa sheria

Amesema Mahakama haiwezi kuwekea maneno Bunge kwa kuwa inaamini kwamba Bunge halisahau na linafahamu wakati linapitisha sheria mpya kuwa kuna sheria ya zamani ambayo pia haijafutwa na hivyo ndio maana kwenye maelezo ya sheria mpya likaweka kipengele kuwa INEC itafanya kazi kwa kufuata sheria itakayotungwa na Bunge.

About The Author

Related Posts