Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Uwekezaji Ofisi ya Msajili Hazina Lightness Mauki amesema uwekezaji wa serikali katika mashirika ya umma nchini umefikia shilingi trioni 86 kufikia mwaka 2024 hivyo amewataka Viongozi wa mashirika ya umma kuhamasisha wananchi wanapata tija kwa uwekezaji huo.
Amesema hayo wakati akifunga Mafunzo kwa viongozi wa Taasisi na Mashirika ya umma nchini walioshiriki mafunzo ya 23 ya Uongozi katika shule ya uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere kwa Mfipa Kibaha Mkoani Pwani akimwakilisha Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu.
Amesema katika mwaka 2023 uwekezaji huo katika Mashirika ya umma umefikia shilingi trioni 64 na kufanya ongezeko la uwekezaji wa shilingi trioni 32 mwaka huu ambao unahitaji umakini mkubwa katika usimamizi ili kuutekeleza katika kuhudumia wananchi.
Amesema viongozi hao wa mashirika ya umma wanatakiwa kuelewa kuwa wao ndiyo chachu ya taifa kubadilika na kufikia malengo yake ya mabadiliko ya kiuchumi kama dunia inavyobadilika na kupiga hatua za maendeleo.
“Sasa kama tunazungumzia uwekezaji huo wa shilingi trioni 86 hivyo na wasimamizi wa mapato ni vema tukajipanga katika kuhakikisha tunasimamia uwekezaji wetu huo mzuri ili ulete tija kwa wananchi amesema Lightness.
Mauki ametaja uwekezaji huo wa fedha ambao serikali imewekeza kuwa upo katika sekta ya zote ikiwa ni pamoja na sekta ya Maji, kilimo, madini na masoko ya fedha.
Aidha amewataka viongozi hao wa mashirika ya umma kujipanga kusimamia uwekezaji huo mkubwa katika nchi ili ulete tija kwa taifa.
“Ni mimi na wewe ndiyo wakuhakikisha wananchi wanapata tija ya kunufaika katika uwekezaji huo mkubwa wa shilingi trioni 86” amesema Lightness.
Malengo ya serikali ni kupunguza hali ya utegemezi wa Mashirika ya Umma kwa serkali nawapa changamoto tunapotoka hapa twende tukawe chachu ya mabadiliko katika Taasisi tunazo zisimamia.
“Tunapaswa kwenda sambamba na falsafa ya Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ya mabadiliko hivyo tuanze kubadilika sasa ili kuleta matokeo chanya” amesema Lightness.
Viongozi hao wamehitimu mafunzo ya Uongozi na Menejimenti kwa viongozi wa Mashirika ya Umma ambayo yamefanyika kwa muda wa siku tano.
“Tunawategemea ninyi ili mkawe chachu ya maendeleo kwenye Taasisi zenu mnazotoka kila mmoja kwa sababu mmepata fursa hii adhimu katika maeneo muhimu hivyo nendeni mkaitumie ipasavyo elimu mliyopata hapa kwa sababu sisi hatuishi kwenye kisiwa twende sambamba na mabadiliko ya kiuchumi sambamba na teknolojia.
“Hivi sasa tumeona kuna mabadiliko ya ya teknolojia ikiwa pamoja na akili mnemba hivyo twende nayo sambamba kama jinsi serikali yetu imeona mabadiliko ni jambo muhimu katika nyanja zote hivyo viongozi wote kwa pamoja twendeni tukaishi haya mabadiliko na sisi pia tubadilike” amesema Lightness.
Amesema kuwa Mashirika ya Umma yamekua chachu ya mabadiliko ya uchumi nchini na ni vema tujipange kusimamia uwekezaji.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Shule ya Mwalimu Nyerere Prof. Marcelina Chijoriga amsema kuwa wahitimu hao wakiwa kwenye mafunzo yao pia wamesoma somo la uzalendo na kusisitiza kuwa kila Mtanzania anatakiwa asome somo hilo pamoja na somo la Usalama wa Taifa kwa sababu viongozi hao ambao wanapokea miradi mingi na kukutana na mambo mbalibali hivyo suala la usalama wa taifa Bi muhimu zaidi katika kujenga uchumi.
“Tumejaribu kuwaambia wanapaswa kuwa na mahusiano mazuri na wadau wanaofanya nao kazi kwani inawezekana ukawa Mkurugenzi Mtendaji mzuri lakini pale linapokuja suala la kujieleza wengi hushindwa ni imani yetu mara baada ya mafunzo haya watakuwa wameiva kiutendaji kwenye nyanja zote.
Prof. Chijoriga amesema kuwa katika shule hiyo wanatoa mafunzo kwa viongozi mbalimbali na kwa upande wa Taasisi za Umma wamelenga kuwabadilisha viongozi wake kutokana na umuhimu wake wengi mmeona baadhi ya mashirika yamekufa na mengine hayafanyi vizuri.
Amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwabadilisha viongozi hao wa umma ili walete ufanisi katika utendaji kazi wao.
Chijoriga amesema kuwa viongozi wa taasisi na mashirika ya umma endapo hawatapata mafunzo hawataweza kuboresha utendaji kazi wao hasa ikizingatiwa kuna mambo mbalibali yanabadilika hivyo nao waendane na hali halisi.
Naye Mwenyekiti wa Wahitimu Simion Marwa amesema kupitia mafunzo hayo, wamejifunza nyenzo mbalimbali za kiutendaji kwa maslahi ya Taifa na bara zima la Afrika kwa ujumla, Ulinzi wa Taifa na Umajumui. Tumejifunza jinsi harakati za ukombozi na mikakati iliyotumika kufikia malengo ya ukombozi.
“Tumejifunza jinsi uongozi na usimamizi wa kimkakati katika mageuzi ya kiuchumi na kijamii unavyoweza kuongeza ufanisi wa taasisi zetu. Ili kuongeza tija na ufanisi, mipango ya kimkakati lazima ieleweke kwa kipindi husika. Tunapotafuta fursa ni lazima kutanguliza maslahi ya Taifa.”
“Vile vile maarifa tuliyopata katika uendeshaji wa mashirika yalenge kwenye ubunifu, uwajibikaji, uaminifu, nguvu ya pamoja katika utendaji, usawa, uwazi na uhuru katika uongozi wa kimkakati” Alisema Marwa.