Wanafunzi Hazina wang’ara siku ya UN

Na Mwandishi Wetu

WANAFUNZI wa shule ya Kimataifa ya Msingi Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam, wameonyesha umahiri mkubwa kwenye siku ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa kutoa mada zilizowavutia wageni waalikwa.

Wanafunzi hao walialikwa kutoa mada kwenye sherehe za miaka 79 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa (UN) ambapo Waziri wa Ulinzi, Stegomena Tax alikuwa mgeni rasmi mwishoni mwa wiki.

“Wanafunzi wetu walialikwa kufanya wasilisho la miaka 79 ya  kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa na waliwasilisha  kuhusu kazi zinazofanywa na Umoja wa Maifa na Mashirika yaliyoko chini yake na kuwashukuru kwa kazi kubwa wanayofanya na wageni walifurahishwa sana na wasilisho,” alisema mwalimu Nikisi Banda aliyeambatana na wanafunzi hao kwenye siku hiyo ya UN.

“Wanafunzi wetu wamefanya vizuri sana na kwa kweli wageni wote waliokuwa wakisimama kuzungumza waliwapongeza kwa namna walivyowasilisha mada ya kwa ufasaha,” alisema

Mgeni rasmi kwenye sherehe hizo, Waziri wa Ulinzi Dk. Stegomena Tax alifurahishwa na ujasiri wa wanafunzi hao kwa kufanya wasilisho ambalo linaonyesha kuwa wanafunzi hao wamesheheni maarifa.

Aliwashauri viongozi wa UN kutumia wasilisho liliotolewa na wanafunzi hao kwaajili ya kuelimisha jamii kuhusu mambo mbalimbali yanayofanywa na shirika hilo kwenye maeneo mbalimbali duniani.

Aliwapongeza wanafunzi wa Hazina kwa kazi nzuri waliyofanya kuandaa wasilisho hilo na namna walivyofanya uwasilishaji kwa umahiri wa hali ya juu.

Wanafunzi hao walimudu kuyaelezea mashirika makubwa yaliyoko chini ya Umoja wa Mataifa ambayo ni UNICEF, UNFPA, UNIC, FAO, UNDP, UNESCO, IFAD, ILO, IOM, UNEP, UN WOMEN, UNAIDS, UNCDF, UNHCR, UNIDO, WFP na  WHO

Mwisho

Related Posts