Na Ludovick Kazoka, Dodoma.
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) Erwin Telemans wa Shirika la Light for the World (LFW) leo ametembelea Kliniki ya Macho ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kujionea huduma za macho.
Ndugu Telemans ameahidi kuwa Shirika lake litaendelea kusaidia huduma za macho za BMH.
“Tunapaswa kuendelea kusaidia huduma za Afya ikiwemo kuwafikia wananchi wanaoishi mbali na wasio na uwezo,” amesema CEO wa LFW wakati akiongea na uongozi wa BMH.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, amesema dhamira ya BMH ni kuifanya Hospitali hii ya Kanda ya Rufaa kuwa kitovu cha huduma za macho nchini.
“Tunaelewa kuwa Light for the World mna mipango mingi, lakini tunaamini mtaipa Tanzania kipaumbele kwenye mipango yenu,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa BMH.
Aidha Mkuu wa Idara ya Macho wa BMH, Daktari Bingwa wa Macho, Jacinta Feksi, amesema BMH inahudumia takribani watu milioni 14 kutoka Kanda ya Kati na mikoa ya jirani.
“Kuwa katikati ya nchi kunawezesha wananchi kutoka kila kona ya nchi kuweza kuifikia BMH,” amesema Dkt Jacinta.
Mwezi Julai, Shirika la LFW liliongeza udhamini wa miaka mitano kwa BMH kupitia Kliniki yake ya Macho kwa ajili ya kufanya huduma mkoba (outreach), mafunzo na vifaa tiba vya macho.