Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini, Choe Son Hui, amewasili siku ya Jumanne katika mji wa mashariki mwa Urusi, Vladivostok, na anatarajiwa kutembelea Moscow siku ya Jumatano, kulingana na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.
Choe aliwasili siku moja baada ya NATO kusema kuwa vikosi vya kijeshi vya Korea Kaskazini vimetumwa nchini Urusi kusaidia vita dhidi ya Ukraine, ingawa Rais wa Urusi Vladimir Putin hajakanusha uwepo wa wanajeshi hao.
Pentagon imekadiria kuwa wanajeshi 10,000 wa Korea Kaskazini wametumwa kwa mafunzo mashariki mwa Urusi, ikiwa ni ongezeko kutoka wanajeshi 3,000 waliokadiriwa wiki iliyopita.
Seoul imekuwa ikiishutumu Korea Kaskazini kwa muda mrefu kuipatia Urusi silaha ili kuendeleza vita vyake dhidi ya dhidi ya Ukraine.
Soma pia: NATO: Wanajeshi wa Korea Kaskazini tayari wako Urusi
Mashaka haya yaliongezeka baada ya kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kusaini makubaliano ya ulinzi wa pamoja na Rais wa Urusi Vladimir Putin mwezi Juni, na kusababisha madai kuwa Pyongyang ilikuwa na mpango wa kutuma wanajeshi kuingia Urusi.
Lavrov: Mkataba na Korea Kaskazini ni halali
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov, alisisitiza siku ya Jumatatu kuwa makubaliano hayo ya kimkakati hayavunji sheria za kimataifa.
“Mkataba wetu wa ushirikiano wa kimkakati na Korea Kaskazini uko wazi na umechapishwa hadharani, ukifuata kikamilifu sheria za kimataifa,” alisema Lavrov.
“Unajumuisha msaada wa pande zote iwapo taifa mojawapo litashambuliwa, na hii inaonyesha msimamo wetu wa uwazi na uaminifu.”
Ingawa Korea Kaskazini imekana kutuma wanajeshi, naibu waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo alisema hivi karibuni kuwa iwapo kutakuwa na utumaji huo, utakuwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Soma pia: Rutte: Naweza kuthibitisha uwepo wa wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Urusi
Kauli hii ndiyo ilikuwa ya kwanza kutoka Pyongyang kuhusu uwezekano wa kushiriki kwa wanajeshi wake, jambo ambalo limeongeza hofu katika jumuiya ya kimataifa.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameonya kuwa Korea Kaskazini huenda hivi karibuni ikawa na wanajeshi 12,000 nchini Urusi.
Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, aliuita utumaji huo wa wanajehi kuwa upanuzi hatari wa vita vya Urusi na ishara ya kukata tamaa kwa Putin, wakati akithibitisha kupelekwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini katika mkoa wa Kursk magharibi mwa Urusi.
Wakati huo huo, maafisa wa Ukraine wamesema leo kuwa takriban watu wanne wameuawa na wengine sita kujeruhiwa katika mashambulizi ya usiku ya Urusi kwenye miji ya Kharkiv na Kyiv.
Mashambulizi hayo yalijumuisha mabomu na droni, huku jeshi la Ukraine likisema limedungua droni 26 kati ya 48 zilizorushwa usiku huo.