Maelfu wakwama kufanya mtihani darasa la saba

 

WANAFUNZI 25,875 waliopaswa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka 2024, hawakufanya mtihani huo. Anaripoti Restuta James, Dar es Salaam … (endelea).

Aidha, watahiniwa 907,429 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa kupata daraja A, B na C na 323,345 wamepata daraja D na E.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Said Ally Mohammed, ameyasema leo tarehe 29 Oktoba 2024, jijini Dar es Salaam alipokuwa akitangaza matokeo ya mtihani huo.

Amesema watahiniwa 1,230,774, walisajiliwa kufanya mtihani huo na kwamba idadi ya ambao hawajafanya ni sawa na asilimia mbili.

Amesema watahiniwa 907,429 waliofaulu kwa daraja la A, B na C, wasichana ni 666,597 sawa na asilimia 54 na wavulana 564,177 sawa na asilimia 46.

Amesema waliopata ufaulu wa juu wa madaraja A na B, ni 431,689 wakiwamo wasichana 216,568 sawa na asilimia 50.1 na wavulana 215,121 sawa na asilimia 49.9.

“Ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.29, na kufikia asilimia 80.87 mwaka huu, kutoka asilimia 80.58 mwaka jana.

Ufaulu katika masomo yote sita umeendelea kuimarika. Ubora wa ufaulu umeimarika kwa asilimia tisa na kufikia asilimia 36 kutoka asilimia 27 mwaka jana,” amefafanua.

Dk. Mohamed amesema wavulana wamewapiku wasichana katika ufaulu wa jumla kwa asilimia 82 na 80, mtawalia.

About The Author

Related Posts