Raia takriban 34 wa Palestina wameuwawa kufuatia shambulio la lililolenga jengo moja la ghorofa tano walikokuwa wakijihifadhi Wapalestina wasiokuwa na makaazi,kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Waliouwawa kaskazini mwa Gaza leo Jumanne katika shambulio la jeshi la Israel wengi walikuwa ni wanawake na watoto kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza.Soma pia: Israel yasema ilimuuwa afisa wa Hezbollah aliyetarajiwa kuwa kiongozi wa kundi hilo
Miongoni mwao ni mama na watoto wake watano na mama mwingine na wanawe sita huku wengine wakiwa ni watu wazima. Shambulio hilo limefanywa katika mji wa Beit Lahiya ulioko karibu na mpaka na Israel ambako pia watu 20 walijeruhiwa.
Jeshi la Israel,ambalo limekuwa likiendesha operesheni kubwa katika eneo hilo la Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza kwa zaidi ya wiki tatu halikutowa tamko mara moja kuhusu mashambulio hayo. Israel imekuwa ikisema kwamba operesheni yake hiyo inalenga kuwasambaratisha wanamgambo wa Hamas inayosema wamejipanga upya kwenye eneo hilo.
Khofu ya Wapalestina
Wapalestina wanakhofia Israel,inatekeleza mpango maalum uliopendekezwa na kundi la majenerali wa zamani wa kijeshi waliotaka wapalestina kaskazini mwa Gaza kupewa amri ya kuondoka na misaada izuiwe kupelekwa kwenye eneo hilo na yeyote atakayekaidi kuondoka atazamwe kama mwanamgambo.
Hata hivyo Israel imekanusha tuhuma hizo,Ingawa siku ya Jumatatu bunge la nchi hiyo lilipitisha sheria mbili ambazo huenda zikazuia shirika la Umoja wa Mataifa linalowasaidia wakimbizi wakipalestina UNRWA- kutoendesha shughuli zake katika ardhi ya Wapalestina.
Jeshi la Israel pia mara kwa mara inaelezwa kwamba katika miezi ya hivi karibuni limekuwa likishambulia maeneo wanakojihifadhi raia walioachwa bila makaazi huku likisema mashambulio yake yamekuwa yakilenga maeneo walikojificha wanamgambo wa Hamas na kudai limekuwa likijaribu kuepuka kuwadhuru raia.Soma pia: Misri yapendekeza kusitishwa mapigano kwa siku mbili Gaza
Hezbollah yapata kiongozi mpya
Mbali na mashambulio hayo ya Gaza huko Lebanon,kundi la wanamgambo la Hezbollah limetangaza kumchaguwa Sheikh Naim Kassem aliyekuwa naibu kiongozi wa kundi hilo,kuwa sasa kiongozi wake mpya anayerithi nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Hassan Nasrallah aliyeuwawa katika shambulio la Israel mwezi uliopita.
Taarifa ya Hezbollah imesema baraza lake la maamuzi linalofahamika kama Shura, limemchagua Kassem ambaye amekuwa kwa miongo akimsadia Nasrallah kama naibu wake. Kundi hilo ambalo pia linapambana na jeshi la Israel, limeapa kuendeleza sera zilizoachwa na Nasrallah hadi utakapopatikana kile ilichokiita Ushindi.
Pamoja na hayo takriban watu 60 wakiwemo watoto wameuwawa katika mashambulio ya Israel yaliyolenga eneo la Mashariki mwa Lebanon Jana Jumatatu kwa mujibu wa wizara ya afya ya Lebanon.Maeneo 12 yalishambuliwa kwenye mikoa ya Baalbek-Hermek na Bekaa, huku watu 58 wakijeruhiwa.
Jana,Jumatatu pia mazungumzo kuhusu usitishaji vita Gaza ya wajumbe wa ngazi za juu yalisitishwa baada ya kufanyika kwa siku mbili huko Doha nchini Qatar huku timu ya wajumbe wa Israel wakirejea nyumbani.