Haya ni licha ya maandamano makubwa ya upinzani uliodai uchaguzi huo si halali na kwamba kulikuwa na wizi wa kura.
Orban, mshirika wa karibu wa Rais Vladimir Putin wa Urusi katika Umoja wa Ulaya, ndiye kiongozi wa kwanza wa kigeni kuizuru Georgia kufuatia uchaguzi wa Jumamosi iliyopita ambao tume ya uchaguzi nchini humo inasema ulishindwa na chama tawala Georgian Dream Party.
Hakuna aliyesema uchaguzi ulikuwa na dosari
Rais wa Georgia, Salome Zourabichvili pamoja na upinzaniwanasema kulikuwa na wizi wa kura kwa usaidizi wa Urusi. Umoja wa Ulaya na Marekani wametoa wito wa uchunguzi kufanyika.
Zourabichvili ambaye ni mkosoaji mkubwa wa chama tawala cha Georgian Dream Party, ametaka jamii ya kimataifa iongeze shinikizo kwa ajili ya kuangaziwa upya kwa uchaguzi huo wa bunge.
Ila Orban ametoa mtazamo tofauti baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Georgia Irakli Kobakhidze ambaye alimpongeza kwa ushindi.
“Nampongeza waziri mkuu kwa ushindi wake wa uchaguzi. Natazama mjadala ulioibuka kuhusiana na uchaguzi huu, nilisoma yaliyoandikwa na mashirika ya kimataifa na nikaona hakuna hata mmoja anayetilia shaka uhuru na demokrasia iliyokuwepo katika uchaguzi huu. Licha ya ukosoaji wote wanaotoa, hakuna anayethubutu kusema hivyo,” alisema Orban.
Haya yanafanyika wakati ambapo tume ya uchaguzi wa Georgia Jumanne imesema itahesabu kura kwa mara nyengine katika asilimia 14 ya vituo vya kupigia kura, baada ya waangalizi huru kutilia shaka jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa.
Kusitishwa kwa ushirikiano wa serikali
Rais Zourabichvili lakini amepuuzilia mbali hatua hiyo ya tume ya uchaguzi akisema hatarajii mabadiliko yoyote akidai tume hiyo iko mikononi mwa chama tawala. Rais huyo wa Georgia amesema mbali na shinikizo la kimataifa, njia nyengine ya kuhakikisha haki inapatikana ni kurudiwa kwa uchaguzi.
Wakati huo huo, Sweden imesitisha ushirikiano wa ngazi ya serikali na Georgia kutokana na hatua ya serikali ya Georgia kuyawekea vikwazo mashirika ya kiraia. Waziri wa biashara za kigeni wa Sweden Benjamin Dousa ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa, uamuzi huo wa kusitisha ushirikiano na serikali ya Georgia ulifanyika wiki iliyopita.
Dousa ameongeza kuwa serikali ya Sweden imeongeza msaada wake kwa mashirika ya kiraia ya Georgia kwa dola milioni 2.3.
Matokeo rasmi ya uchaguzi wa bunge Georgia yanaonyesha kuwa chama cha Georgian Dream Party kilishinda uchaguzi kwa karibu asilimia 54, hiyo ikiwa zaidi ya kura laki tatu zaidi ya vyama vinne vya upinzani kwa pamoja.